BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kusafiri kuelekea nchini Kenya Disemba 2 kwa ajili ya michuano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itakayofanyika katika mji wa Mombasa kuanzia Disemba 4 hadi 14.

Msafara wa timu ya Bunge utahusisha watu 60 ambapo michezo sita ndiyo itashindaniwa ambayo ni soka, mpira wa pete, mpira wa wavu, riadha, kuvuta kamba, kikapu na gofu.

Mwenyekiti wa timu ya Bunge William Ngeleja alisema kwa sasa kikosi chao kipo kambini jijini Tanga kujiweka sawa kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ambayo wamejinasibu kushinda michezo yote sita.


Ngeleja alisema maandalizi ya timu yao yanaendelea vizuri na kuwaahidi Watanzania kuwa watafanya vizuri kutokana na na kikosi imara walicho nacho.

"Tuna matumaini makubwa ya kushinda kila mchezo tutakaoshiriki kutokana na uimara wa vikosi vyetu mfano timu yetu ya Netball ndiyo Bingwa wa mara zote ilizoshiriki na haikuwahi kupoteza mchezo wowote," alisema Ngeleja.

Naye Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Nape Nnauye alisema hana hofu na timu hiyo na ana imani kubwa ya kufanya vizuri huku akiwataka wadau mbali mbali kujitokeza kuisaidia kwenye maandalizi kuhakikisha vikombe vyote sita vinakuja nchini.

Michuano ilianzishwa mwaka 2001 ambapo mwaka huu nchi zote sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitashiriki. Mwaka jana timu ya Bunge haikushiriki kutokana na kashkashi za uchaguzi mkuu.

Post a Comment

 
Top