BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MASHINDANO ya kuchezea mpira 'Football Freestyle' yaliyoandaliwa na chama cha mchezo huo Freestyle Football Tanzania (FFT) yanatarajiwa kuanza Novemba 19 kwa Wilaya tatu za Jiji la Dar es Salaam ambazo ni Temeke, Ilala na Kinondoni, uzinduzi wa mashindano hayo utafanyika viwanja vya Mwembe Yanga.

Mgeni rasmi kwenye mashindano hayo yanayodhaminiwa na kinywaji cha Red bull ikishirikiana na Clouds TV kupitia kipindi cha Sports Bar anatarajiwa kuwa Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea.

Mratibu wa shindano hilo Jacob Mbuya aliwaambia Waandishi wa Habari kuwa washiriki hawatalipa kiasi chochote cha fedha kama kiingilio ambapo washiriki wanatakiwa kuwa na umri kuanzia miaka 15 na kuendelea.

Fomu za ushiriki zinapatikana Clouds TV na Ofisi za chama hicho zilizopo Kinondoni pamoja na mitandao ya kijamii kupitia kurasa zao."Mashindano haya yataanza jijini Dar es Salaam kwa Wilaya tatu ambapo Wilaya za Temeke na Ilala zitazoa washiriki watano kila moja huku Kinondoni ikitoa sita ambao wataingia Fainali itakayochezwa Coco Beach, Disemba 11," alisema Mbuya na kwamba Ilala yatafanyika viwanja vya Boma, Novemba 26 kabla ya kuelekea Kinondoni kwenye uwanja wa  Tp Sweet Corner, Disemba 3.

Mbuya alizitaja baadhi ya sheria za mchezo huo kuwa ni kila mshiriki atapewa sekunde 30 za kuchezea mpira, mchezaji atakuwa peke yake jukwaani na pia akidondosha mpira atakuwa amepoteza pointi.

Post a Comment

 
Top