BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima

WASOMAJI wa mtandao wa BOIPLUS wamemchagua, Haruna Niyonzima wa Yanga kuwa kiungo aliyeisaidia zaidi timu yake kwenye mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu huu.

Katika mechi tano za mwisho za mzunguko wa kwanza Niyonzima amekuwa kwenye kiwango bora na kuisaidia timu yake kufanya vizuri kwa kupunguza idadi ya pointi  kutoka nane hadi kufikia pointi mbili dhidi ya vinara Simba wenye pointi 35 kwenye msimamo wa ligi huku wao wakishika nafasi ya pili kwa pointi 33.

Niyonzima amepata kura 1405 sawa na asilimia 63 na kumshinda kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto aliyepata kura 756 sawa na asilimia 27 ambapo awali alikuwa akiongoza kabla ya raia huyo wa Rwanda kugeuza matokeo na kumwacha kwa kura nyingi.


Kura zikionyesha ushindi wa Niyonzima  
Wengine waliokuwa kwenye kinyang'anyiro hicho cha wiki moja ni Kenny Ally (Mbeya City), Shaban Kisiga (Ruvu Shooting) na Abubakar Salum 'Sure Boy' (Azam).

BOIPLUS ambayo ni tovuti ya habari za michezo na burudani ipo kwenye mchakato wa kuandaa shindano kubwa zaidi ambalo litaambatana na zawadi mbalimbali kwa washindi.

Wachezaji watakaoingia kwenye kinyang'anyiro hicho watateuliwa na jopo la makocha kabla ya kupigiwa kura na mashabiki wao ambao ni wasomaji wa mtandao huu shindano ambalo litakuwa likifanyika kila baada ya miezi miwili na kumtangaza mshindi.

Post a Comment

 
Top