BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
Jeshi la Polisi nchini limewatia nguvuni watuhumiwa watano wanaotajwa kuhusika na mauaji ya bondia Thomas Mashali kilichotokea usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam.

Mashali alifikwa na mauti hiyo baada ya kushambuliwa na watu wasiofahamika huko Kimara Bonyokwa  ambapo alipigwa kichwani majeraha yaliyopelekea kuondoa uhai wake akikimbizwa hospitali ya Rufaa, Muhimbili.

Habari kutoka kwa ndugu wa marehemu, Emmanuel Mashali zilisema kuwa watuhumiwa wawili walikamatwa eneo la Kimara Bonyokwa wakati watatu wakikamatwa Kimara Saranga.

"Tumewakamata hawa watuhumiwa kwenye maeneo mawili tofauti, Kimara Bonyokwa na huko Kimara Saranga ingawa mmoja amejileta mwenyewe kwenye gari la polisi, kitakachofuata Jeshi la Polisi ndilo litajuwa maana tunawaachia wao wachukue hatua za kisheria," alisema Emmanuel.

Kamanda wa Polisi Kanda ya Kinondoni, Suzan Kaganda alisema kuwa jeshi linaendelea na upelelezi na watakapokamilisha upelelezi ndipo watatoa taarifa kamili ingawa alieleza kuwa baada ya Mashali kufariki kesi hiyo itageuzwa kuwa kesi ya mauaji na si kesi ya shambulio la kuzuru mwili.

Mashali anatarajiwa kuzikwa kesho kwenye makaburi ya Kinondoni saa saba mchana ambapo mwili wake huenda ukaagwa kati ya viwanja vya Shule ya Msingi Tandale ama viwanja vya Leaders. Kikao cha mapromota wa ngumi nchini kinachoendelea ndicho kitaamua eneo la kumuaga kati ya maeneo hayo mawili.

Post a Comment

 
Top