BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
WINGA wa Simba, Peter Mwalyanzi ameonywa kutorudi uwanjani hadi hapo 
atakapopona kabisa majeraha ya nyama za paja na kuna hatari ya kutocheza mechi 
zote za mzunguko wa pili endapo hatazingatia masharti aliyopewa na daktari wake.

Mwalyanzi anayekipiga kwa mkopo katika timu ya African Lyon alijitonesha 
majeraha hayo wakati timu yake ikicheza na Stand United, mjini Shinyanga ikiwa 
ni mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom.

Mwalyanzi aliiambia BOIPLUS kuwa awali aliumia nyama hizo akiwa Simba na hivi sasa ni mara ya pili hivyo Dr Gilbert Kadyage ambaye ni mtaalamu wa misuli kwa wanasoka mbalimbali nchini, amemtaka kukaa nje ya uwanja hadi hapo atakaporuhusiwa ikiwemo kutojihusisha hata na mazoezi ya aina yoyote.


"Nasumbuliwa na nyama za paja, haya ni majereha ambayo niliyapata tangu nikiwa Simba hapa ni kama nimejitonesha, nilianza kucheza kabla hata sijapona vizuri jambo ambalo lilikuwa kinyume na masharti niliyopewa na daktari wangu na sasa ameniambia nikianza kucheza kabla sijawa sawa basi naweza kukosa mechi zote za msimu huu," alisema Mwalyanzi.

Akifafanua juu ya majeraha ya mchezaji huyo, Dr Kadyage alisema, "Majeraha ya kuchanika kwa nyama za paja kupona kwake kunategemea na 
ukubwa wa tatizo husika, ila ni rahisi sana mchezaji kupona haraka kama anafuatilia matibabu. Huwa inachukuwa hata wiki tatu kama atakuwa mhudhuriaji mzuri wa kliniki.

"Mwalyanzi anaweza kuchukuwa muda mrefu kupona kwasababu tu mahudhurio 
yake ya kliniki si mazuri, anaweza kuja leo halafu akaja baada ya siku kadhaa, 
itamchukuwa muda, na pia hatakiwi kurudi uwanjani haraka kama alivyofanya hapo awali na jeraha lake la sasa ni kovu la kidonda cha mwanzo hivyo anapaswa kuwa makini," alisema Dr Gilbert.

Dr Gilbert alisema mara nyingi kuchanika nyama za paja huwa kunawapata zaidi 
wachezaji wenye vimo vifupi kwani misuli yao huwa migumu na matibabu yake ni kuhudhuria kliniki mfululizo pamoja na kusinga 'massage'.

Post a Comment

 
Top