BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

INAWEZA kuwa ni mkwara tu ama ni ukweli kwamba Ruvu Shooting wameweka wazi kesho Jumatano hawatapeleka timu yao uwanjani kucheza na Yanga kwani wachezaji wao wamechoka na safari na wakigoma kweli basi watapokwa pointi na kushushwa daraja.

Mechi hiyo ya mwisho katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu kwa timu hizo imepangwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam ambapo Ruvu wameingia saa 4 asubuhi na kikawaida timu inapaswa kucheza mechi nyingine baada ya saa 48 kupita tangu icheze mechi ya awali.

Hata hivyo, Ruvu Shooting wakigomea kweli kuipeleka timu uwanjani basi Yanga watapewa ushindi wa bao 2-0 na pointi tatu huku wao wakikumbwa na adhabu ya kushushwa daraja kwani hadi sasa Bodi ya Ligi haijajibu ombi lao la kusogeza mechi hiyo mbele, ombi ambalo waliliwasilisha jana Jumatatu.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire ameiambia BOIPLUS kuwa wapo tayari kukabiliana na adhabu yoyote itakayotolewa na Bodi ya Ligi ila msimamo wao ni kutopeleka timu uwanjani wachezaji wao wamechoka na safari hiyo ndefu.


Masau Bwire

"Wachezaji nao ni binadamu, wameingia saa nne asubuhi ya leo watachezaje kesho, tumetuma maombi Bodi ya Ligi kwamba mechi yetu tunaomba ichezwe Alhamisi ya Novemba 11 kama ilivyokuwa hapo awali ila hakuna majibu wanayotupa basi acha iwe itakavyokuwa.

"Hatutapeleka timu na tupo tayari kwa hatua yoyote watakayotuchukulia ila wanapaswa kuangalia sisi wengine tumesafiri kwa umbali gani na miundombinu yetu ipoje, nimewasiliana na mtu pale Bodi ya Ligi alisema tusubiri lakini hadi sasa hakuna jibu lolote," alisema Masau na kuongeza.

"Hii mechi imebadilishwa mara nne, ilitakiwa ichezwe Novemba 9, ikapelekwa mbele hadi Novemba 11, ikarudishwa  nyuma Novemba 10  na sasa itachezwa kesho inaonyesha hata wao Bodi ya Ligi hawajajipanga," alisema.

Ruvu Shooting ilikuwa Bukoba kucheza na Kagera Sugar ambako waliambulia kichapo cha bao 3-1 wakati Yanga nao walikuwa Mbeya kucheza na Prisons walikotoka na ushindi wa bao 1-0. 

Timu zote zilicheza mechi juzi Jumapili ila zilitofautia katika usafiri, Yanga wamerudi na Ndege ili wachezaji wao wasichoke na waweze kucheza mechi hiyo wakati Ruvu wenyewe wamerudi kwa kutumia usafiri wa barabara ambapo wamesafiri kwa siku mbili.

Post a Comment

 
Top