BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umesema upo tayari kuchezeshwa na waamuzi kutoka nje ya nchi kwenye mechi yao na  watani wao wa jadi Simba endapo Shirikisho la Soka nchini (TFF) litaridhia.

Juzi, Msemaji wa Simba, Haji Manara aliweka wazi kuwa hawataingiza timu uwanjani dhidi ya Yanga endapo mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini kwa madai kuwa hawatendewi haki na huwapendelea Yanga.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga amewaambia Waandishi wa Habari kuwa kama TFF itakubali ombi la Simba mechi yao kuchezeshwa na waamuzi kutoka nje ya Tanzania hawatakuwa na pingamizi ila ametoa angalizo kuwa tukio hilo litashusha hadhi ya marefarii nchini.

Sanga alisema waamuzi wanafanya kazi kubwa za kutafsiri sheria 17 za soka na pia sio kazi rahisi kama watu wanavyochukulia hivyo TFF inatakiwa kufanya maamuzi sahihi kuelekea jambo hilo.

"TFF wakikubali tukicheza na Simba mchezo uchezeshwe na waamuzi kutoka nje hatuna shida ila wanatakiwa kulitazama kwa umakini suala hili kwakuwa linaweza kuleta mpasuko kwenye soka letu," alisema Sanga.

Jana, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas aliwaonya Simba kuacha jaribio la kutoingiza timu uwanjani kama hakutakuwa na waamuzi kutoka nje kwakua ni kosa kwa mujibu wa kanuni za ligi kitu kitakachopelekea kupata adhabu kubwa.

Wakati huo huo kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini Jumatatu ijayo tayari kwa maandalizi ya mzunguko wa pili wa ligi.

Post a Comment

 
Top