BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
PRISONS ipo kwenye mchakato wa kusaka washambuliaji wawili ambapo mapendekezo yao ya kwanza yalikuwa kwa Malimi Busungu ila dili hilo limebuma kwani Yanga wamedai kuendelea kumtumia hivyo Wajelajela hao wamekuwa kwenye wakati mgumu kwani bado hawajaona straika mwingine mzoefu wa kumsajili.

Mapendekezo hayo yanakuja baada ya mfungaji bora wao wa msimu uliopita, Jeremiah Juma kusumbuliwa na goti aliloumia wakati wa mechi yao na Mbeya City ambapo imeelezwa haijajulikana ni lini atarejea uwanjani kwani anaendelea na matibabu.

Msimu uliopita, Jeremiah aliifungia timu hiyo mabao 15 huku akisaidiana na mshambuliaji mwenzake Mohamed Mkopi ambaye anatumikia adhabu ya kufungiwa kwa mwaka mmoja kutoshiriki soka kwa kosa la kusaini mkataba na Mbeya City wakati ana mkataba na Prisons. Mkopi alifunga mabao matano.

Katibu Mkuu wa Prisons, Oswarld Morris amesema kuwa walipeleka maombi yao kwa uongozi wa Yanga lakini waligoma kuwapa mchezaji huyo aliyesajiliwa akitokea Mgambo JKT na hajacheza mechi hata moja ya ligi kuu msimu huu. Timu kama Mtibwa Sugar na Stand United nazo ni miongoni mwa timu zilizokuwa zinafukuzia saini ya Busungu ila zote zimemkosa mchezaji huyo.

"Ni lazima tutafute washambuliaji wawili wazoefu, tulimlenga Busungu ila mpango umeharibika, hatuna washambuliaji kwasasa kwani Jeremiah bado anaumwa na huwezi kulazimisha kumwingiza uwanjani kwa kipindi hiki mpaka apone kabisa, kikubwa tunachokifanya kwake ni kuendelea kumjenga kisaikolojia maana majeraha yamemkosesha amani, tuna wachezaji wazoefu na wenye nguvu," alisema Morris.

Akizungumzia kwa upande wa mkataba wa kocha Meja Mstaafu Abdul Mingange, Moris alisema kuwa; "Ni kweli mkataba wake umekwisha na hatujafanya mazungumzo yoyote ya kumwongeza mkataba kwani hiyo ni kazi ya mabosi wetu, tunawasubiri hao ndipo tutajuwa nini tufanye ama kitu gani kinaendelea,".

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi ni miongoni mwa makocha waliokuwa wanatajwa kutua Prisons ingawa Morris ameshindwa kulizungumzia zaidi hadi hapo mabosi wake watakapokutana.

Post a Comment

 
Top