BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
RAIS wa Klabu ya Simba, Evans Aveva amekanusha taarifa ya kutaka kumsajili kiraka Mbuyu Twite aliyeachwa Yanga kwakuwa hana nafasi ndani ya kikosi cha sasa cha Kocha Joseph Omog.

Twite hakuwepo kwenye mchezo maalum wa kumuaga uliochezwa jana Jumamosi dhidi ya JKU na Yanga kulala kwa mabao 2-0 hali iliyozua minong'ono ya kuwa nyota huyo atajiunga na Wekundu hao katika dirisha dogo linaloelekea ukingoni.

Siku chache baada ya Yanga kutangaza kumuacha nyota huyo na kumsajili kiungo Justin Zulu kutoka Zesco ya Zambia kumekuwa na tetesi kwenye mitandao ya kijamii kuwa Twite anaelekea Simba lakini Aveva amesema kwamba mchezaji huyo hayumo kwenye mipango yao kutokana na kuwa na nyota wenye vipaji zaidi yake.

Aveva alisema "Nasikia kuna taarifa kuwa kuna mchezaji ameachwa na Yanga anaitwa Mbuyu anakuja kwetu taarifa hizo sio kweli wala hatuna mpango naye tutasajili nyota wengine lakini sio yeye,".


Miaka minne iliyopita Twite alisaini mkataba wa awali na Simba ambapo alishaandaliwa hadi jezi kwenye uongozi wa Mwenyekiti Ismail Aden Rage kabla ya kutimkia Yanga hali iliyoleta taharuki ambapo mashabiki wa klabu hiyo wamekuwa wakimzomea kila mara.

Aveva alisema ripoti ya Kocha wao imeonesha anahitaji kipa na tayari wamemsajili Daniel Agyei kutoka Medeama na kiungo James Kotei huku ikihitaji mshambuliaji ambaye atasaidiana na Laudit Mavugo pamoja na Ibrahim Ajib.

Simba itashuka dimbani kesho Jumatatu kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Chamazi Complex kujiweka sawa kabla ya mechi yao ya kwanza ya mzunguko wa pili dhidi ya Ndanda FC wikiendi ijayo.

Post a Comment

 
Top