BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
TIMU ya Azam FC imethibitisha kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza Januari mosi visiwani Zanzibar huku ikijinasibu kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Azam imepangwa kundi moja na timu za Yanga na Zimamoto ambalo linatarajiwa kuwa gumu kutokana na uimara wa timu zote hasa zinazotoka huku bara.

Ofisa Habari wa klabu hiyo Jaffar Iddi Maganga amewaambia Waandishi wa Habari kuwa mashindano hayo yatamsaidia Kocha Zeben Hernandez kuendelea kuwatumia wachezaji wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili lililopita ili wazoeane kabla ya kuanza mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

"Tunathibitisha kushiriki michuano ya kombe la Mapinduzi ambapo timu inatarajia kuondoka kati ya tarehe 30 na 31 kuelekea visiwani humo tayari kwa mashindano hayo," alisema Maganga.

Maganga pia alisema kikosi chao kinaendelea kujifua kwa ajili ya mchezo wao wa ligi siku ya  Alhamisi dhidi ya Tanzania Prisons utakaopigwa kwenye uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamazi.

Mchezo huo utakuwa ni wa kwanza katika mzunguko huu wa pili kucheza nyumbani baada ya kutoka sare mechi mbili dhidi ya African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1) zote wakiwa ugenini.

"Tumejipanga kuhakikisha tunautumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani kupata pointi tatu muhimu dhidi ya Prisons baada ya kutoka sare michezo miwili mfululizo ugenini" alisema Maganga.

Mchezo huo utapigwa saa usiku jioni katika dimba hilo.

Post a Comment

 
Top