BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Chamazi

KLABU ya Azam imefanikiwa kuanza vema maisha mapya bila makocha wahispaniola baada ya kuichapa Prisons bao 1-0 kwenye mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliopigwa kwenye dimba la Azam Complex.

Bao pekee la vijana hao wa kocha mzawa Iddi Cheche aliyekabidhiwa jukumu hilo jana baada ya Zeben Hernandez na benchi zima la ufundi kutimuliwa, lilifungwa na nahodha John Bocco dakika ya 40 kwa shuti kali baada ya kuwahadaa walinzi wa Prisons.

Katika mchezo huo Azam walionyesha kiu kubwa ya ushindi kwa kufanya mashambulizi mengi ingawa uimara wa kikosi cha Prisons ulikuwa kikwazo cha wao kupata mabao zaidi.


Prisons walianza kulishambulia lango la Azam wakitafuta bao la kusawazisha lakini wakapata pigo dakika ya 69 baada ya mchezaji Kazungu Mashauri kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia rafu mbaya aliyomchezea kiungo wa Wanalambalamba hao, Joseph Mahundi ambaye hakuweza kuendelea na mchezo.

Ushindi huo umewafanya Azam wachupe hadi nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 30 sawa na Kagera Sugar wakiwazidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Simba wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 44 huku Yanga wakishika nafasi ya pili na pointi zao 40.


Post a Comment

 
Top