BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Chamazi
BAADA ya Yanga na Simba kusajili nyota kadhaa kutoka nchini Zimbabwe hali ni tofauti kwa Azam FC ambao wao wameingia nchini Ghana na kusajili nyota watano ambao wataitumikia timu hiyo mzunguko wa pili wa ligi utakaonza kesho.

Azam imefanya zoezi maalum la kuwatambulisha wachezaji hao wapya zoezi lililoambatana na dua kwa ajili ya kuhakikisha mzunguko wa pili wanafanya vizuri na lengo lao ni kunyakuwa ubingwa licha yakuwa nyuma kwa pointi 10 dhidi ya vinara Simba.

Wachezaji hao waliotambulishwa ni Yakubu Mohamed, Samwel Affoul, Yahaya Mohamed, Enock Agyei na beki Daniel Amoah wote kutoka Ghana wengine ni Stephani Kingue kutoka Cameroon na Joseph Mahundi aliyetokea Mbeya City.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo Saad Kawemba amewaambia Waandishi wa Habari kuwa mabadiliko yote yaliyofanywa ni kutokana na mapendekezo ya Kocha wao Zeben Hernandez.

"Leo ni siku maalum kwa klabu yetu kuwatambulisha wachezaji wetu wapya tutakaokuwa nao kuanzia mzunguko wa pili wa ligi utakaonza kesho na hayo yanatokana na mapendekezo ya mwalimu," alisema Kawemba.

Kawemba amewataja wachezaji walioachwa kuwa ni Pascal Wawa na Michael Baloue waliokuwa huru, Ya Thomas, Fransisco Zekumbawira pamoja na Jean Baptiste Mugiraneza ambao mikataba yao imevunjwa huku stahiki zao zikiwa tayari zimefanyika.

Wachezaji waliotolewa kwa mkopo ni Bryson Raphael (Mbeya City), Ame Ally (Kagera Sugar), na Kelvin Friday (Mtibwa) huku wakimrudisha kundini beki Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda FC kwa mkopo.

Azam watashuka dimbani siku ya Jumapili kumenyana na African Lyon katika mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa ligi.

Post a Comment

 
Top