BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
KLABU ya Azam leo imefanikiwa kuingia mkataba na wachezaji watatu, beki wa kati Yakubu Mohammed, kiungo mkabaji Stephan Kingue Mpondo na winga Joseph Mahundi.

Zoezi hilo la kuingia mikataba hiyo lilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba, Meneja Mkuu  Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez na Meneja wa timu Phillip Alando.

Mohammed amesaini mkataba wa miaka mitatu akitokea Aduana Stars ya Ghana akiziba nafasi ya Pascal Wawa huku Mpondo anayetokea Coton Sports ya Cameroon akisaini mwaka mmoja.


Katika kuongeza makali kwenye eneo la ushambuliaji Azam  imemrejesha winga wake wa zamani aliyekulia kwenye Academy yao Joseph Mahundi ambaye amesaini miaka miwili akitokea Mbeya City baada ya  kumaliza mkataba wake. 

Wakati huo huo, Azam imethibitisha taarifa ya kufikia makubaliano ya kuachana na kiungo mkabaji raia wa Rwanda Jean Baptiste Mugiraneza ‘Migi’ ambaye amepata timu nchini Vietnam na muda wowote kuanzia sasa atakwenda huko.


Azam inamtakia mafanikio mema Migi huko aendako na inapenda kumkaribisha muda wowote atakapojisikia kurejea tena na katika kuziba nafasi yake wamemsajili Mpondo ambaye alikuwa nahodha wa timu ya Taifa ya Cameroon kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika nchini Rwanda mwanzoni mwa mwaka huu.

Post a Comment

 
Top