BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

TIMU ya Azam FC kesho asubuhi itasafiri kwa basi kuelekea mkoani Ruvuma tayari kwa mchezo dhidi ya Majimaji katika muendelezo ligi kuu ya Vodacom utakaofanyika Uwanja wa Majimaji mjini Songea Jumamosi ijayo.

Azam ina safiri ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na African Lyon kwenye mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi.

Katika mchezo huo Azam itawakosa wachezaji watatu ambao ni beki Abdallah Kheri, kiungo Mudathir Yahaya wote wakiwa wagonjwa huku Gardiel Michael akiendelea na matibabu ya mkono wake wa kushoto ambao umeteguka.

Kocha Mkuu wa Azam  Zeben Hernandez alisema kuwa ametumia programu ya leo kuwaunganisha wachezaji huku akidai kuwa maandalizi makubwa watayafanya wakifika Songea kutokana na muda kubana.


“Tunatarajia kufanyia kazi na kurekebisha udhaifu ulioonekana kwenye mchezo uliopita kikubwa tutajitahidi  kupata ushindi kwakua ndiyo malengo yetu kurejea na pointi tatu,” alisema Hernandez.

Zeben aliongeza kuwa kwenye mchezo uliopita walifanikiwa kucheza vizuri lakini hawakuwa na bahati ya kuweza kufunga mabao huku akidai kuwa anatarajia kulifanyia kazi suala hilo ili lisiweze kujitokeza katika mechi inayokuja.

“Kama uliona wachezaji waliweza kufanya mashambulizi mengi langoni mwa wapinzani walijitahidi kupiga mashuti, safu yetu ya ulinzi haikupata shida sana na ilikuwa imara muda wote wa mchezo jambo ambalo tulilikosa duru ya kwanza,” alisema Hernandez.

Azam wamefanikiwa kujikusanyia pointi 26 kwenye ligi wakiwa nafasi ya tatu baada ya kushinda mechi saba, sare tano na kupoteza michezo minne ambapo inazidiwa pointi 12 na vinara Simba wenye alama 38 huku Yanga iliyonafasi ya pili ikijizolea 36.

Post a Comment

 
Top