BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
NI miezi miwili sasa imepita tangu serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo izifungie timu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa baada ya mashabiki wao kufanya uharibifu kwa kung'oa viti na kuvunja mageti.

Simba ilipigwa marufuku hadi pale ambapo watafanya matengenezo ya viti vilivyong'olewa na mashabiki wake ambapo tayari uongozi wa klabu hiyo ulianza ukarabati na kesho Jumamosi Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo Nape Nnauye atakwenda kukagua maendeleo ya ukarabati huo.

Endapo Simba nao watakuwa wamemaliza kufunga viti hivyo kuna uwezekano mkubwa na wao kusaini mkataba wa makubaliano kama ilivyo kwa Yanga ambao leo wameruhusiwa kutumia Uwanja huo katika mechi zao za kitaifa na kimataifa. Yanga wao walitakiwa kutengeneza mageti manne yaliyokuwa yamevunjwa na tayari walitengeneza.

Yanga leo Ijumaa imesaini mkataba huo jijini Dar es Salaam chini ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Elisante Ole Gabriel huku Yanga ikiwakilishwa na Kaimu Katibu Mkuu, Baraka Deusdedit.

Yanga wamesaini mkataba huo na kuruhusiwa kuutumia uwanja wa Taifa pamoja na wa Uhuru kwa sharti la kuvitunza viwanja hivyo, mali na vyote ndani ya viwanja hivyo kwa kipindi chote ambacho watakuwa wakivitumia na kama uharibifu utatokea watakuwa na jukumu la kugharamia ukarabati.

Wizara hiyo pia imeitaka Yanga kuwa tayari kugharamia kila kitu endapo uharibifu utafanywa na mashabiki ama wachezaji wao kwenye mechi yoyote ile.

Kama Serikali itakuwa imeridhika na ukarabati huo uliofanywa na Simba basi mechi ijayo ya watani kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom itakayochezwa Februari mwakani basi itachezwa hapo huku Simba wakiwa wenyeji wa Yanga.

Habari ambazo BOIPLUS inazo ni kwamba tayari Simba walimaliza zoezi la ufungaji viti hivyo 1781.

Post a Comment

 
Top