BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

DURU la Pili la Ligi Kuu ya Vodacom litaanza kutimua vumbi kesho Jumamosi kwa viwanja vinne nyasi zake kuwa kwenye wakati mgumu huku kipute hicho kikiendelea keshokutwa, Jumapili.

Mabingwa watetezi wa taji hilo Yanga itakuwa mgeni wa JKT Ruvu ya mkoani Pwani mchezo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Licha ya kwamba mwenyeji wa mchezo huo ni Ruvu ambayo uwanja wake wa nyumbani ni Mabatini ulioko Mlandizi lakini kwa mujibu wa Kanuni ya 6 (5) na (6) ya Ligi Kuu Bara mechi zake za nyumbani dhidi ya Simba, Yanga na Azam  hufanyika Uwanja wa Uhuru.

Michezo mingine ya kesho ni Kagera Sugar kuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya wakati Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini ilihali Mwadui  itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Mwadui Complex.

Jumapili, Ndanda itakuwa mwenyeji wa Vinara wa ligi, Simba kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku Mbao FC  ikicheza na Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kirumba wakati African Lyon  itaikaribisha Azam FC katika Uwanja wa Uhuru huku Majimaji itakuwa Mbeya kucheza na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa masharti kadhaa likitaka klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kufuata masharti yafuatayo; 

Klabu kutumia makocha wenye sifa kwa mujibu wa kanuni ya 72 ya Ligi Kuu ya Vodacom ambapo makocha wanaopaswa kukaa kwenye benchi msimu huu wasipungue sifa ya kuwa na leseni B ya CAF.

Pia kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza na Pili masharti ni lazima makocha wawe na sifa za kuzinoa timu hizo ambazo zimeainishwa kwenye kanuni za ligi husika.

TFF imeagiza klabu kutotumia wachezaji wa kigeni au makocha kama hawana vibali vya  kufanyia kazi kutoka Idara ya Uhamiaji nchini iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.

Post a Comment

 
Top