BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
NAHODHA wa timu ya Azam FC John Bocco ‘Adebayor’, anaamini  kikosi chao kitakuwa bora zaidi kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara utaokaonza Disemba 17 kutokana na usajili walioufanya kwenye dirisha dogo.

Bocco alisema kuwa morali waliyokuwa nayo wachezaji pamoja na nguvu za nyota wapya walioongezwa kikosini kwenye usajili huu utaweza kuwasaidia kufanya vizuri.

“Tunamshukuru Mungu tumeweza kufanya mazoezi salama kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili  wachezaji wote tuna morali tumerudi kuhakikisha tunaisaidia timu yetu kufanya vizuri,” alisema Bocco.

Nahodha huyo aliongeza kuwa: “Ukizingatia hata katika usajili kuna wachezaji tumewaongeza kwa hiyo nina imani tutaweza kujituma na Mungu atatusaidia kuweza kufanya vizuri mzunguko wa pili.”


Benchi la Ufundi kwa kushirikiana na Uongozi wa timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo unaoendelea umewasajili nyota wawili kutoka Ghana, Yahaya Mohamed aliyetokea Aduana Stars na staa wa Sekondi Hasaacas, Samuel Afful.

Pia imeweza kuwarudisha kundini wachezaji wake wawili waliokuwa kwa mkopo, beki wa kati kinda Abdallah Kheri aliyekuwa Ndanda na winga wa kushoto Enock Atta Agyei (Medeama).

Azam imemaliza mzunguko wa kwanza wa ligi ikiwa imekujikusanyia pointi 25 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo ikizidiwa alama 10 na vinara Simba wenye pointi 35 huku Yanga akiwa wa pili baada ya kufikisha alama 33.

Post a Comment

 
Top