BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

DAKTARI wa klabu ya Simba Yassin Gembe amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu afya ya kiungo wao mpya James Kotei kuwa anaendelea vizuri na leo ameanza mazoezi pamoja na wenzie.

Kotei alitolewa uwanjani dakika ya 19 kwenye mchezo walioibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC juzi Jumapili baada ya kugongwa mdomoni  hali iliyopelekea kushindwa kuendelea na mechi.

Gembe ameiambia BOIPLUS kuwa Kotei anaendelea vizuri na leo amefanya mazoezi pamoja na wenzake ambapo mwalimu akiona inafaa anaweza kumtumia kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu utakaofanyika Jumamosi ijayo uwanja wa Uhuru.

"Alichanika kidogo mdomoni baada ya kupigwa kiwiko na mchezaji wa Ndanda na tayari amepata matibabu yuko fiti leo amefanya mazoezi na wenzake" alisema Gembe.

Kabla ya kuumia Kotei aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo lililopita akitokea nchini Ghana aliichezea Simba mechi mbili za kirafiki dhidi ya Polisi Moro na Mtibwa Sugar na kuonyesha kiwango safi kilicho wapa imani kubwa mashabiki wa Wekundu hao ambao wana hamu ya kunyakua ubingwa walioukosa kwa misimu minne sasa.

Nyota huyo anaungana na nahodha Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Mohamed Ibrahim na Mwinyi Kazimoto kutengeneza safu imara ya kiungo ya timu ya Simba.

Post a Comment

 
Top