BOIPLUS SPORTS BLOG

Nihzrath Ntani Jr
    NI  nyakati za usiku mwingi, pembezoni mwa pwani ya Mediterrania, ndani ya mji wa Middlesbrough nchini England ndani ya moja ya klabu maarufu kati ya zilizopo katika eneo hilo.

  Watu ni wengi sana usiku huu mahali hapo. Wakaka na wadada wakicheza muziki kwa madaha. Watu wanaburudika kweli kweli. Ni kama  wapo katika dunia isiyo na shida.

   Mbele ya steji katika ukumbi huo, mwanaume mmoja anaonekana akichezea vyombo vya muziki kwa ustadi mkubwa huku akitikisa kichwa kwa maringo akifuatilia mapigo ya muziki huo. Masikio yake yamezibwa na 'Headphone' . Bila shaka huyu ni 'DJ' usiku huu.

  Ni nani mtu huyu? Najiuliza kisha naanza kurejelea kumbukumbu zangu. Naam! miaka 42 iliyopita DJ huyu alizaliwa katika jiji la Bilbao ndani ya jimbo la Basque nchini Hispania. Historia yake imejaa mizaha mingi. Mizaha yenye kuchekesha.

DJ MENDIETA.....hii ndio kazi ambayo Mendieta aliipenda tangu akiwa mdogo, na sasa anaifanya baada ya kustaafu soka

  Akiwa kijana mdogo, ndoto ya mtu huyu ilikuwa kuja kuwa mwanariadha maarufu Duniani ama DJ maarufu siku moja. Akiwa na miaka 14 tu Mendieta aliacha kucheza soka na kujiingiza katika mchezo wa riadha ili kutimiza ndoto hiyo.

  Uamuzi wake wa kuacha soka uliwasononesha sana wazazi wake. Lakini hawakuwa na budi kumuunga mkono mtoto wao kwa uamuzi wake huo. Lakini alipofikisha miaka 16, DJ huyu wa usiku huu aliamua kuacha mchezo wa riadha na kujiunga tena na soka.

  Ni uamuzi huu uliokuja kumpa umaarufu duniani kote miaka michache baadae. Mtu huyu anaitwa Gaizka Mendieta.

  Majina mengi yamepita klabuni Valencia lakini ndani ya mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo katu hawawezi kumsahau fundi huyu wa kihispaniola.

  Unaikumbuka Valencia yenye watu kama Santiago Canizares, Kily Gonzalez, Claudio Lopez, Ruben Baraja, David Albelda, Jocelyn Angloma, Amedeo Carbon, Pablo Aimar, Zahovic na wengine wengi kikiwa chini ya kocha Hector Cuper?.

Nahodha wa kukumbukwa ndani ya Valencia

  Kikosi hicho kiliongozwa na nahodha Mendieta. Akiwa na uwezo wa kucheza namba yoyote katika eneo la kiungo cha kati. Alisaidia sana kuifikisha  Valencia katika fainali mbili mfululizo za mabingwa wa ulaya, wakifanya hivyo katika msimu wa 1999/2000 na 2000/01 wakipoteza dhidi ya Real Madrid kabla hawajaadhibiwa na Bayern Munich kwa njia ya matuta.

  Umahiri wa Mendieta ulikuwa ukishangaza wengi maana alikuwa fundi kweli kweli wa mpira. Kwa wakati huu naburudika kumtazama Luca Modric ama Andres Iniesta lakini miaka 15 iliyopita burudani ya Modric na Iniesta ilikuwa ikipatikana toka kwa Mendieta pekee.

  Uwezo wa kupiga pasi zenye macho, kusaidia kukaba, ubunifu, uwezo wa kupiga mashuti nje ya 18 zilikuwa sifa kuu za Mendieta. Haikuwa ajabu kupitia umahiri wake, shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kumtangaza kuwa kiungo bora barani Ulaya kwa miaka miwili mfululizo.

   Akiwa Valencia alitwaa mataji mbali mbali likiwemo taji la Copa del Rey. Ilipofika Julai 1, 2001, nyota huyo alifanya uamuzi ambayo alikuja kuujutia baadae pale alipohama Valencia na kwenda Lazio ya Italia kisha kuwa miongoni mwa wachezaji ghali zaidi Duniani kwa wakati huo.

Siku Mendieta alipotambulishwa katika klabu ya Lazio

  Uamuzi huo ulikuwa kama kujimaliza mwenyewe huku akitupilia mbali ofa kutoka Real Madrid na Barcelona. Alipowasili Lazio alikutana na viungo wawili waliojenga himaya yao klabuni hapo. Viungo hao ni Paved Nedved na Juan Sebastian Veron. Ikawa ngumu kupenya katikati yao.

  Alitumia miaka matatu klabuni hapo huku muda mwingi akiwekwa benchi na ilipofika  2004. Mendieta alikubali kwenda Barcelona kwa mkopo ambako pia hakuweza kuteka mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo. Msimu mmoja baadae alielekea nchini England kunako klabu ya Middlesbrough.

  Alitumia misimu minne klabuni hapo huku akiwa sehemu ya timu iliyoweka rekodi ya kutwaa taji la ligi kwa mara ya kwanza katika historia ya Middlesbrough.

  Ilipofika Mei 13, 2008 Mendieta alitangaza kustaafu baada ya kukumbwa na majeruhi yasiyokwisha na kupelekea kushuka kwa kiwango chake na kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.

  Baada ya kustaafu Mendieta aliamua kuishi nchini England katika mitaa ya Yarm ndani ya mji wa middlesbrough.

Mendieta akifanya kazi ya uchambuzi wa soka

  Kwa sasa Mendieta anajihusisha na uchambuzi wa soka kupitia kituo cha Sky Sports cha uingereza, akichambua mechi za La Liga. Pia akitumia muda wake wa ziada kufanya kazi ya uDJ katika kumbi mbalimbali ikiwa moja ya kazi aliyoipenda sana akiwa mdogo. 

Thank You Gaizka Mendieta. 

Tukutane tena jumamosi ijayo katika ukurasa huu wa "THE LEGEND" hapa hapa BOIPLUS.

Maoni;
+255713414189
ntaniy97@gmail.com

Post a Comment

 
Top