BOIPLUS SPORTS BLOG

LONDON, Uingereza

VIGOGO Chelsea, Manchester United na Arsenal wote wamepata ushindi na kuwapatia zawadi mashabiki wao katika siku hii maalumu ya kufungua zawadi (Boxing Day).

Chelsea imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza baada ya kuichapa AFC Bournemouth mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Chelsea wamefikisha pointi 46 wakifuatiwa na Liverpool wenye alama 37 sawa na Arsenal wakitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa huku majogoo hao wakishuka dimbani kesho Jumanne kuwakabili Stoke City.

Pedro Rodriguez aliifungia Chelsea mabao mawili dakika za 24 na 90 huku Eden Hazard akifunga jingine kwa mkwaju wa penalti dakika ya 49.


United imeshinda mchezo wa nne mfululizo baada ya kuwafunga vibonde Sunderland wanaonolewa na kocha wa zamani wa Mashetani hao, David Moyes kwa mabao 3-1 mechi iliyopigwa uwanja wa Old Trafford.

Magoli ya United yalifungwa na Daley Blind, Zlatan Ibrahimovic na Henrik Mkhitaryan na kufikisha pointi 33 lakini wameendelea kubaki nafasi ya sita.

Olivier Giroud aliinusuru Arsenal kupata sare baada ya kufunga bao pekee dakika ya 87 dhidi ya West Bromwich Albion nakupanda hadi nafasi ya tatu na kuishusha Manchester City ambayo itacheza na Hull City usiku huu.


Kocha mpya wa Crystal Palace, Sam Alladyce amekaribishwa na sare ugenini dhidi ya Watford huku mshambuliaji wake Christian Benteke akikosa mkwaju wa penalti.

Matokeo kamili ya mechi zilizochezwa leo 

Watford 1-1 Crystal Palace
Arsenal 1-0 West Bromwich
Bunley 1-0 Middlesbrough
Chelsea 3-0 AFC Bournemouth
Leicester City 0-2 Everton
Man United 3-1 Sunderland
Swansea City 1-4 West Ham

Post a Comment

 
Top