BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, Dar
KIPA wa zamani wa Simba na Mbeya City, Juma Kaseja na beki Mohamed Fakih wapo safarini kuelekea mkoani Kagera kwa ajili ya kujiunga na Kagera Sugar. Wachezaji hao kesho Ijumaa watasaini mkataba wa miezi sita kila mmoja.

Msimu uliopita Kaseja aliidakia Mbeya City lakini alishindwa kusaini mkataba mpya kwa mali kauli na sasa amekwenda Kagera ambako atachukuwa nafasi ya Hussein Sharif 'Casillas' aliyesimamishwa kwa tuhuma za kuhujumu timu ilipocheza na Yanga.

Casillas na mwenzake Erick Kyaruzi walihusishwa na tuhuma hizo timu yao ilipopokea kichapo cha bao 6-2 ambapo hukumu yao imedaiwa kuwa huenda ikasomwa baada ya sikukuu ya Krismasi. 

Fakih aliomba kuvunja mkataba na Simba kutokana na kushindwa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza ili kulinda kipaji chake na baadaye kwenda African Lyon ambako pia walishindwa kumalizana kwa upande wa pesa ya usajili.

Katibu Mkuu wa Kagera Sugar, Hamisi Madaki ameiambia BOIPLUS kuwa wamemaliza mazungumzo na wachezaji hao na kilichobaki ni kuwapa mikataba tu huku akiweka sababu za kumchukuwa Kaseja kwamba atasaidia kwani ni mzoefu na amesomea ukocha.

"Ni kweli wachezaji hao tutaingia nao mikataba kesho baada ya kuwasili huku nia yetu ni kuongeza nguvu kikosini kutokana na uzoefu walionao, wote ni mapendekezo ya kocha Mecky Mexime na hatuwezi kuendelea kusubiri hatima ya Casillas bila kuwa na mbadala, ndio maana tumemsajili Kaseja," alisema Mdaki.

Akifafanua zaidi juu ya mikataba hiyo mifupi Madaki alisema kuwa, "Wachezaji wenyewe wameomba kupewa mikataba ya aina hiyo ili kwanza wazoee mazingira na sisi tuwasome vizuri kama wataridhika basi tutawaongeza hapo baadaye,".

Post a Comment

 
Top