BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
MWENYEKITI wa Baraza la Wadhamini la Klabu ya Simba, Hamis Kilomoni, ameweka wazi kuwa alimwambia mfanyabiasha maarufu nchini, Mohamed Dewji 'Mo' kuwa asisaini nyaraka yoyote ndani ya klabu hiyo hadi hapo mchakato huo utapokamilika na majadiliano ya pamoja kufikiwa vingine atakuwa amepoteza haki zake.

Mo ameonyesha nia ya kuwekeza ndani ya Simba kwa Sh 20 bilioni huku akitaka amiliki hisa asilimia 51 jambo ambalo linapingwa na baadhi ya wanachama wakihofu kupoteza haki ya umiliki wa klabu yao.

Mzee Kilomoni alisema kuwa wakati huu ambao mchakato ulikuwa unaendelea Mo alikwenda nyumbani kwa mzee huyo aliyewahi kuwa mchezaji, Katibu mkuu wa Sunderland ambayo sasa ni Simba ambaye ndiye ana Hati ya jengo la Simba kuomba ushauri wa nini kifanyike ili aweze kuwekeza.


"Mo alikuja hapa nyumbani kwangu na tulizungumza mambo mengi sana, sikatai Mo awekeze ila nataka kufahamu ni kwa mfumo gani, maana tusikurupuke tu bila kuelewa, wengi nadhani hawaelewi juu ya hili na ndiyo maana nilimtaka Mo asithubutu kusaini nyaraka yoyote atakayopewa na viongozi wa Simba.

"Nilimshauri kwamba kama atakutana nao na kujadili basi wajadili ila asisaini mpaka majadiliano hayo yaletwe Baraza la Wadhamini tuyapitie kama ni kuyabadili,kuyafanyia marekebisho, kuyakubali ama vinginevyo," alisema na kuongeza.

"Hili suala bado linasubiri majadiliano ila kama amesaini nyaraka yoyote inaweza kumpotezea haki zake kama hatutafikia kule anakokuhitaji yeye, kwani jambo kama hili linapaswa kupitia hatua kwa hatua tena za kisheria," alisema Mzee Kilomoni.

Mzee huyo pia alisema kwa niaba ya viongozi wenzake wa Baraza la Udhamini, wamepinga Mkutano Mkuu wa dharura ulioitishwa kwa mujibu wa Katiba ya Simba kwamba ni batili kwani haujafuata taratibu za kikatiba huku Rais wa Simba, EvansAveva kesho Jumamosi akitarajia kugawa nyaraka kwa viongozi wa matawi ili kupitia ajenda za mkutano huo.Hata hivyo, Katiba ya Simba haijaweka wazi majukumu na mipaka ya Baraza la Udhamini ambalo lipo kwa ajili ya kusimamia mali za klabu hiyo kama linahusika kwenye maamuzi ya kuitisha ama kuzuia mkutano mkuu bali Ibara ya 22 inampa mamlaka Rais na Kamati Kuu ya Utendaji kuitisha mkutano mkuu wa dharura.

Ibara ya 22 (1) kinasema 'Rais wa Klabu kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Utendaji anaweza kuitisha Mkutano Mkuu wa Dhararu kama anaona inafaa'. Ibara 22 (3) kinasema 'wito wa mkutano mkuu hauna budi kupelekwa angalau siku 15 kabla yamkutano ulioitishwa na kamati ya utendaji' ambapo Aveva ametekeleza hili.

Ibara 22 (4)  kinaeleza kuwa 'Ajenda na nyaraka nyingine muhimu zitapelekwa kwa wajumbe angalau siku saba kabla ya mkutano'. Jambo ambalo limepangwa kufanywa kesho Jumamosi.

Kilomoni alisema viongozi wa Simba wakifuata utaratibu ndipo waitishe mkutano huo vingine kutatokea vurugu kwani tayari wanachama wamegawanyika hivyo imani ya nchi inaweza kupotea.

Post a Comment

 
Top