BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma,Dar
KOCHA wa African Lyon, Charles Otieno raia wa Kenya ameshangazwa na benchi la ufundi la timu ya Azam kuchelewa kuwaingiza nyota wazawa kwenye mechi yao jana Jumapili ambao walionyesha uhai mkubwa kwa matajiri hao baada ya kuingia.

Azam iliwacheza nyota watano wa kigeni Yakubu Mohamed, Yahaya Mohamed, Bruce Kangwa, Steven Kingue na Samwel Affoul ambao hawakucheza vizuri kwa kile kilichoonekana kuwa ni ugeni wa mazingira na kutoizoea ligi.

Kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bila kufungana kipindi cha pili Azam iliwaingiza Frank Domayo, Aboubakari Salum 'Sure boy' na Ramadhan Singano ambao walibadilisha kabisa radha ya mpira na kuwa na madhara makubwa langoni mwa Lyon kwa muda mrefu.

Otieno alisema kuchelewa kufanywa kwa mabadiliko hayo ilikuwa ni ahueni kwa Lyon kwani nyota hao walipoingia muda mwingi lango lao lilitawaliwa na kashkashi ambazo zingeweza kuzaa mabao kama kungekuwa na muda wa kutosha.

"Wale wachezaji wazawa waliongia kipindi cha pili walikuwa na madhara makubwa kuliko walioanza nashangaa makocha wa Azam kwanini waliwachelewesha kuwaingiza naamini wangewahi ingekuwa shida sana kwa upande wetu," alisema Otieno.

Mara kadhaa, Kocha mkuu wa Azam Zeben Hernandez ambaye alikuwa jukwaani kutokana na kutumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu alikuwa akiwasiliana na wasaidizi wake kwa simu kuwapa maelekezo kutokana na wachezaji wake kukosea hasa wanapofika golini kwa Lyon jambo ambalo lilikuwa likimtia hasira.

Otieno alisema pia nyota wapya waliosajiliwa na Azam ambao watano kati yao wametokea nchini Ghana wakipewa muda wa kukaa pamoja na kuzoea mazingira ya ligi watakuwa na mchango mkubwa kwa timu kwakua wana uwezo mzuri.

Post a Comment

 
Top