BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR

UONGOZI wa klabu ya Simba uliona isiwe tabu wakati wanahitaji huduma ya mshambuliaji Pastory Athanas jana Alhamis wakaamua kumalizana na klabu yake ya zamani Stand United kwa kuilipa Sh 10 milioni ikiwa ni fidia za kuvunja mkataba wake uliokuwa umebaki mwaka mmoja na nusu.

Uongozi wa Stand ulitishia kuweka pingamizi Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuzuia mchezaji huyo kuichezea Simba kwa kile kilichoelezwa kuwa ana mkataba mrefu na Simba hawakufuata taratibu za usajili badala yake walikwenda kumalizana na mchezaji kabla aya uongozi wake.

Habari kutoka ndani ya Stand United, zilisema kuwa uongozi wa Simba uliwasiliana na viongozi wa Stand kabla ya dirisha kufungwa na kutumwa majina hayo TFF na kuomba kulipa fidia hiyo ambapo Stand walitaka walipwe Sh 15 milioni ingawa baadaye walikubali kushuka.

"Walichokifanya Simba ni kuzungumza na mchezaji huku wakimpa mkataba bila kuja kwetu viongozi, tulikutana na kujadili kwamba kama Simba wasingekuja basi Pastory asingeenda popote hadi amalize mkataba ila kwasasa hakuna tatizo atacheza Simba," alisema kiongozi huyo.

Pastory ni miongoni mwa wachezaji wanne wapya waliosajiliwa kwenye kikosi cha Simba akiwemo kipa Daniel Agyei, kiungo James Kotei waliotoka Ghana pamoja na Juma Luizio atakayecheza kwa mkopo wa miezi sita akitokea Zesco.

Simba imewatema wachezaji wawili kipa Vincent Angban na Musa Ndusha huku wakiwapeleka kwa mkopo Awadh Juma, Malika Ndehule waliokwenda Mwadui FC pamoja na Emmanuel Semwanza aliyekwenda Majimaji, mshambuliaji Ame Ally amerudi kikosini kwake Azam.

Post a Comment

 
Top