BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
KOCHA mkuu wa Yanga, George Lwandamina atakutana kwa mara ya kwanza na Wekundu wa Msimbazi Simba inayofundiswa na Mcameroon Joseph Omog Februari 18 kwenye mechi ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Vodacom ambao ratiba yake imetolewa leo hii na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).

Katika mchezo wao wa mzunguko wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao moja huku mechi hiyo ikitawaliwa na vurugu zilizopelekea viti 1,781 vya uwanja wa Taifa kung'olewa na mashabiki wanaosadikika kuwa ni wa Simba baada ya kutoridhishwa na maamuzi ya refarii Martin Saanya.

Mshambuliaji Amisi Tambwe aliifungia Yanga bao la uongozi dakika ya 26 kwa mpira ambao ulionekana kumgonga mkononi kabla ya kufunga huku akishindwa kuliona tukio hali iliyoleta taharuki ambapo nahodha wa Simba Jonas Mkude alizawadiwa kadi nyekundu. Shiza Kichuya aliwasawazishia Wekundu hao dakika ya 88.

Jonas Mkude

Mzunguko wa pili utaanza Disemba 17 ambapo Simba itakuwa ugenini dhidi ya Ndanda FC huku Yanga wakicheza dhidi ya JKT Ruvu kwenye uwanja Uhuru jijini Dar es Salaam.

Ligi hiyo itasimama kwa wiki mbili kuanzia Januari mosi kupisha mashindano ya Mapinduzi yanayofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar huku timu tatu kutoka bara zikishiriki ambapo fainali zake zitafanyika Januari 12.

Januari 28 Simba itawakabirisha 'Wanalambalamba' Azam FC kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 kwenye mzunguko wa kwanza.

Post a Comment

 
Top