BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeanza mazungumzo na Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko Muhimbili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa madaktari na wahudumu wa afya michezoni.

TFF ina matumaini kuwa mafunzo hayo yataboresha uwezo wa madaktari hao sambamba na kusambazwa kwa vifaa maalumu vya tiba ya moyo kwenye klabu za soka nchini ili kujua afya za wachezaji kabla ya kuanza kucheza.

Hii ni hatua thabiti inayochukuliwa na uongozi wa TFF baada ya kutokea vifo vinavyosababishwa na mshtuko wa moyo kwa wachezaji ukiwamo ugonjwa wa ‘cardiac arrest’ ambao kwa taarifa za awali unaonyesha ndio uliosababisha kifo cha mhezaji wa Mbao FC U20, Ismail Mrisho Khalfan.


Marehemu Ismail alifariki dunia baada ya kuanguka uwanjani Disemba 4 kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera wakati timu yake ikicheza na Mwadui katika mechi ya ligi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20.

Kifo hicho kimegusa hisa za wanafamilia wengi wa mpira wa miguu akiwamo Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA) Gianni Infantino ambaye juzi alituma salamu za rambirambi kwa Rais wa TFF Jamal  Malinzi kutokana na kifo cha ghafla cha Mchezaji huyo.

Salaamu za Rais Infantino, zinakwenda sambamba na za Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Nape Nnauye na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou.

Post a Comment

 
Top