BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR
KLABU ya Azam FC imeamua kuachana na winga Hassan Kabunda aliyedaiwa kuwa katika hatua za mwisho kusaini mkataba na matajiri hao na badala yake watampa mkataba wa miaka miwili kiungo Joseph Mahundi ambaye ameanza mazoezi na timu hiyo leo Jumatatu asubuhi.

Mahundi atasaini mkataba wake kati ya kesho Jumanne au Jumatano mbele ya Meneja wake Herry Mzozo ambaye kwasasa yupo safarini Mbeya ingawa awali kocha wa timu hiyo Zeben Hernandez ndiye aliyekuwa akisubiriwa kumsainisha Mahundi baada ya kutoka kwenye mapumziko mafupi.

Mahundi ameonekana kwenye mazoezi hayo yaliyofanyika Uwanja wa Chamazi ambao ni mali ya klabu hiyo tajiri nchini iliyoanza kujiandaa kwa ajili ya mechi za mzunguko wa pili wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza Disemba 17.

Wakati Mahundi aliyeichezea Mbeya City kwa mwaka mmoja na nusu akisubiri kumwaga wino klabu hiyo imeamua kuachana na Kabunda wa Mwadui Fc baada ya kuona usajili wake una mlolongo mrefu. Kabunda amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Mwadui hivyo ilikuwa ni lazima mkataba wake uvunjwe kwa kulipa.Kiongozi mmoja wa Azam aliiambia BOIPLUS kuwa, "Kabunda ni mchezaji mzuri ila alijifunga mwenyewe kwa kuchukuwa mkataba mwingine wakati ule wa kwanza hajamaliza matokeo yake bei wanayotaka tuwape ni kubwa ndio maana tumeachana naye,".

Katibu Mkuu wa Mwadui, Ramadhan Kilao alifafanua kuwa, "Azam walienda kuzungumza na mzazi wa Kabunda wakati mchezaji ana mkataba na sisi, hatuna pingamizi naye ila wafuate taratibu hata hao Simba waje tuzungumze kama kweli wanamuhitaji,".

Habari zilizopo ni kwamba baada ya dili la kwenda Azam kushindikana winga huyo anasakwa na Simba ambao pia hawajafikia makubaliano ya kusaini mkataba. Hii itakuwa mara ya pili kwa Simba kuhitaji huduma ya Kabunda ila wanashindwa kuvunja mkataba.

Post a Comment

 
Top