BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

TIMU ya Majimaji imewapa mkataba wa miezi sita kipa Kuitche Bidoul raia wa Ivory Coast aliyechukuwa nafasi ya Amani Simba ambaye ametemwa pamoja na mshambuliaji Kelvin Sabato aliyetokea Stand United huku akiwindwa na Wekundu wa Msimbazi, Simba.

Kuitche aliingia nchini tangu Aprili mwaka huu kwa lengo la kusaini Simba lakini dili lake lilishindikana na hivyo aliendelea kujifua kivyake.

Meneja wa mchezaji huyo, Shomary Ndizi alisema kuwa uongozi wa Majimaji umempa mkataba baada ya kuridhika na kiwango chake kwenye mazoezi aliyoyafanya kwa wiki moja chini ya kocha Kally Ongala.


"Kuitche atakuwa na Majimaji kwa mechi za mzunguko wa pili ndiyo makubaliano ya mkataba yalivyo, wakitaka huduma yake zaidi basi mazungumzo yatafanyika upya," alisema Shomary.

Kwa upande wa Sabato imeelezwa kuwa Jana Jumapili Simba walianza kumsaka ili wampe mkataba lakini Wekundu hao walichelewa kwani tayari mshambuliaji huyo alisaini mkataba na Majimaji, juzi Jumamosi.

Sabato ambaye ni mchezaji pekee aliyefunga hat-trick mzungumzo wa kwanza wa ligi kuu, amesaini mkataba wa miezi sita tu kuichezea Majimaji.

"Hapa sina namna maana tayari nimesaini mkataba na Majimaji lakini Simba wangewahi kidogo ningeenda huko kwani tangu nichukuwe barua ya kuonyesha kuwa nipo huru Stand United nimekaa nayo wiki nzima, nimesaini huko nao ndiyo wanakuja," alisema Sabato.

Post a Comment

 
Top