BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu
TIMU ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Vijana  wenye umri wa chini ya miaka 14, leo  inaanza kambi rasmi katika Hosteli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Vijana hao 22, wanaingia kambini kujiandaa na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Shelisheli unaotarajiwa kufanyika Desemba 17 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ambao una baraka za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu duniani (FIFA), umepangwa kufuata taratibu zote za kimataifa ikiwa ni pamoja na kupigiwa nyimbo za Taifa kwa timu zote sambamba na kupandisha Bendera za Mataifa husika.

Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu  Oscar Mirambo anayepata ushauri kutoka kwa Mshauri Mkuu wa Maendeleo ya Soka la Vijana, Kim Poulsen kinatarajiwa kuwa na michezo minne ya kirafiki ya nyumbani kabla ya kucheza na Shelisheli.

Michezo hiyo ya kirafiki ni dhidi ya Moro Kids ya Morogoro Desemba 8, saa 10.00 jioni kabla ya mchezo wa marudiano Desemba 9  saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Jamhuri na baadaye timu hiyo itarejea Dar es Salaam mchana kujiandaa na safari ya Zanzibar Desemba 11 ambako itakuwa na michezo miwili mingine ya kirafiki.

Zanzibar itacheza na Kombaini ya timu ya Vijana wa Zanzibar Desemba 12,  kabla ya kurudiana Desemba 14, mwaka huu na timu hiyo na Kombaini kabla ya kurejea Bara Desemba 15, kujiandaa na mchezo kirafiki wa kimataifa dhidi ya Shelisheli.

Timu hii inaandaliwa kuja kwa timu mpya ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17  'Serengeti boys' ambao watashiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana mwaka 2019 ambapo Tanzania imeteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa mwenyeji. Kambi itavunjwa Desemba 18.

Post a Comment

 
Top