BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
YANGA imemsajili mshambuliaji wa JKU,  Emmanuel Martin na huenda ndiye amefunga usajili kwa upande wa Mabingwa hao watetezi wa ligi kuu nchini ila mtihani wake mkubwa ni kuhakikisha anawakalisha benchi Amissi Tambwe na Donald Ngoma.

Martin anatakiwa kuhakikisha anapata namba kwenye kikosi hicho tofauti na ilivyokuwa kwa washambuliaji wa timu hiyo ambao wameonekana kuchemsha akiwemo Anthony Matheo, Malimi Busungu pamoja na Paul Nonga aliyeshituka mapema na kuomba kuondoka kwenda Mwadui.

Nonga, Busungu na Matheo ni washambuliaji wazuri lakini hawakufanikiwa kupata namba za kudumu kwenye kikosi cha Hans Pluijm wakati huo akiwa kocha mkuu wa timu hiyo ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi huku kocha mkuu akiwa ni George Lwandamina aliyetokea Zesco ya Zambia.


Usajili wa Martin umekuja baada ya JKU kufanikiwa kuifunga Yanga bao 2-0 katika mechi yao ya kirafiki iliyochezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, huku mabao yote yakifungwa na straika.

Martin ameisaidia timu yake ya JKU kuchukua ubingwa wa visiwani Zanzibar msimu uliopita huku msimu huu akiwa tayari ameshafunga mabao sita akizidiwa mawili na anayeongoza mpaka sasa kwenye ligi hali inayoonyesha kuwa ni mfungaji mzuri ingawa atakumbana na upinzani wa washambuliaji hao wawili wa kigeni.

Usajili huo unafanana na usajili wa Matheo ambaye alifanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Kagame akiwa na timu yake ya zamani ya KMKM na kuwa kivutio kwa timu za Simba na Yanga ingawa Wekundu wa Msimbazi walizidiwa ujanja na Yanga, hata hivyo mara nyingi Matheo amekuwa akikaa benchi na umahiri wake.

Post a Comment

 
Top