BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
MECHI ya leo ya kirafiki kati ya Yanga na JKU ilitangazwa kuwa ni maalumu kwa ajili ya kumuaga mchezaji wao Mbuyu Twite lakini imezua maswali baada ya mchezaji huyo kutokuwepo kabisa uwanjani hapo kama ilivyotarajiwa. Mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa Yanga ulitangaza kuwa mechi hiyo ni maalumu kwa ajili ya kumuaga kiraka huyo  ambaye ameitumikia klabu yao kwa misimu minne sasa huku kocha mpya, George Lwandamina naye akitumia mechi hiyo ya kwanza tangu aajiriwe kuangalia mapungufu ya wachezaji ambao leo wamepokea kipigo cha bao 2-0 dhidi ya JKU.


BOIPLUS ilimuuliza Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusdedit kuhusu kutokuwepo kwa Twite kama ilivyotangazwa ambaye alijibu kwa ufupi, "Hata mimi sifahamu chochote,".

Yanga wameamua kuachana na Twite ambapo nafasi yake imechukuliwa na Mzambia, Justine Zulu aliyetokea Zesco United ambaye alionyesha kucheza soka la taratibu huku akipiga pasi kwa umakini mkubwa kuelekea kwa mawinga ingawa alionekana kuwa mzito tofauti na matarajio ya mashabiki wengi wa soka walivyotarajia.

Yanga iliyowaanzisha wachezaji wengi wa kikosi cha pili ilizidiwa sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza ambapo dakika ya 12 mshambuliaji wa JKU, Emmanuel Martin aliipatia timu yake bao la kwanza baada ya kupokea mpira wa kona fupi uliopigwa na Mbarouk Chande.


Martin alifunga bao la pili dakika ya 27 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nassor Mattar na kumzidi mbinu beki Pato Ngonyani kabla ya kuachia shuti kali lililomshinda mlinda mlango Ally Mustapha 'Bathez'.

Kipindi cha pili kocha Lwandamina alibadili kikosi chote kilichoanza na kuwafanya Yanga kucheza vizuri ambapo walifanya mashambulizi mengi kuliko awali huku mipango ya kutafuta mabao ya kusawazisha ikionekana ingawa haikufanikiwa.

Post a Comment

 
Top