BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
MTIKISIKO uliozikumba Simba, Yanga na Azam kutoka Idara ya Uhamiaji ulikwenda hadi kwenye timu nyingine zote zilizoajiri wachezaji na makocha wa kigeni kwamba hawataruhusiwa kuwatumia hali iliyopelekea leo Ijumaa uongozi wa Mbeya City kuhaha kuwalipia vibali nyota wao ili kesho  Jumamosi waweze kucheza mechi ya dhidi ya Toto African ya jijini Mwanza.

Mratibu Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Idara ya Uhamiaji, Malko Matico jana Alhamisi alisema wanaingia kwenye msako mkali ndani ya timu hiyo na kwamba ikibainika hawana vibali basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kuwazuia kufanya kazi yoyote hapa nchini pamoja na kutozwa faini.

Baada ya tamko hilo, uongozi wa Mbeya City ulioajiri wageni sita ambao ni Kocha Mkuu, Kinnah Phiri, kipa Owen Chaima, Sankhan Mkandawile (Malawi), Titto Okelo, Hood Mayanja na William Otong wote kutoka Uganda wameanza kushughulikia malipo ya vibali vya makazi na kazi ambapo kila mmoja anapaswa kulipiwa dola 2,450.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo, zilisema kuwa uongozi unapambana kuhakikisha tatizo hilo wanalimaliza leo Ijumaa kabla ya mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Sokoine.

"Leo asubuhi wamepiga picha kwa ajili ya kupelekea kwenye fomu za uhamiaji na ndiyo wanahangaikia malipo ili kesho wacheze hiyo mechi," kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, uongozi wa City haukuwa tayari kuweka wazi juu ya mchakato huo kwani Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema kuwa taarifa rasmi ataitoa jioni ya leo Ijumaa ila wanashughulikia.

Post a Comment

 
Top