BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
NYOTA watatu Titto Okello, Hood Mayanja raia wa Uganda pamoja na Zahoro Pazi wanatarajia kumwaga wino kuichezea Mbeya City kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom iliyopangwa kuanza Desemba 17.

Okello na Mayanja wameichezea African Lyon mzunguko wa kwanza na sasa wapo huru baada ya kumaliza mikataba yao kwani walisaini mkataba wa miezi sita kila mmoja huku Zahoro akiwa mchezaji huru.

Okello na Mayanja tayari wapo jijini Mbeya ambapo imedaiwa keshokutwa Jumatatu huenda watasaini mkataba wa mwaka mmoja kila mmoja huku Zahoro akitarajiwa kuondoka kesho Jumapili.

Kwa upande wa Zahoro alishindwa kucheza ligi baada ya FC Lupopo kugoma kutoa ITC yake kwa madai kuwa Zahoro anatakiwa kurudisha pesa zao alizochukuwa wakidai kuwa alisaini mkataba ndipo wakapewa ITC hiyo ambayo hadi sasa haijaachiwa ingawa habari za ndani ni kwamba wameanza upya kuomba ili aweze kucheza.

Zahoro Pazi

Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri aliiambia BOIPLUS kwa njia ya simu kutoka Malawi kwamba endapo uongozi utafanikiwa kuwanasa wachezaji hao atakuwa amemaliza tatizo la safu ya ushambuliaji.

"Kama nilivyosema hapo awali kuwa Okello na Mayanja ni wachezaji wazuri na nimewaona, tayari nilifanya nao mazungumzo ilibaki kumalizana na viongozi kwa upande wa kuwapa mikataba, Zahoro simfahamu pengine pia ni mchezaji mzuri," alisema Phiri.

Phiri anatarajia kutua jijini Mbeya keshokutwa Jumatatu huku akiendelea kusisitiza kwamba anahitaji kipa mzoefu kama Abraham Chove wa Ndanda FC pamoja na beki wa kati ambapo walianza kufanya mazungumzo na Mohamed Fakih aliyetimkia Kagera Sugar.

Katibu Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema kuwa kila kitu kitawekwa wazi mara baada ya kocha kuwasili huku akikiri kufanya mazungumzo ya awali na Zahoro.

Post a Comment

 
Top