BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Dar
Jonas Mkude kulia akipambana na Shiza Kichuya

NAHODHA wa timu ya Simba Jonas Mkude leo amejiunga na wenzake kambini mkoani Morogoro  kujiwinda na mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara ambapo Wekundu hao ndiyo vinara wakiwa na pointi 35.

Kikosi cha Simba chini ya Kocha Joseph Omog na msaidizi wake Jackson Mayanja kilisafiri jana kuelekea Morogoro bila nahodha huyo kutokana na kushughulikia masuala ya kifamilia ambayo ilielezwa kuwa viongozi wa klabu hiyo wana taarifa zake.

Mkude ameiambia BOIPLUS kuwa alishindwa kusafiri na timu jana kutokana na matatizo ya kifamilia huku akiwataka wapenzi na mashabiki wa Simba kushusha pumzi kwakua hajafikiria kuondoka kwa Wekundu hao licha ya watu kuvumisha anataka kuwaacha kwenye mataa.

"Nilishindwa kusafiri na timu jana nilikuwa na matatizo ya kifamilia na viongozi wangu wanajua ila haina uhusiano wowote na maneno yanayosemwa na watu kuwa nataka kuondoka, leo nimejiunga na wenzangu kila kitu kipo sawa".

Kiungo huyo alisema pia mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya yanaendelea vizuri na imani yake watafikia mahala pazuri na kutia saini kandarasi mpya muda si mrefu huku akisema taarifa zinazosemwa kuwa amegoma kuongeza mkataba ni kumchonganisha na mashabiki ambao wanamuamini.

Ukitoa kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya Yanga Oktoba mosi Mkude hajakosa mechi yoyote ya ligi kwenye mzunguko wa kwanza huku akionyesha kiwango kikubwa cha kuwalinda mabeki pamoja na kuanzisha mashambulizi kuanzia katikati ya uwanja.

Katika siku za karibuni baada ya kufunguliwa dirisha hili dogo la usajili kiungo huyo amekuwa akihusishwa na kutaka kujiunga na Yanga kitu ambacho amekipinga kwa nguvu zote akisema suala hilo halipo kabisa akilini mwake.

Post a Comment

 
Top