BOIPLUS SPORTS BLOG

Akram Msangi, Chamazi
LICHA ya kuifungia timu yake bao la kufutia machozi kiungo wa Simba Mohamed Ibrahim alilimwa kadi nyekundu pamoja na Mohamed Banka wa Mtibwa Sugar baada ya kupigana uwanjani.

Mwamuzi Michael Magoli aliwatoa nyota hao dakika ya 85 baada ya kupigana uwanjani baada ya kuchezeana rafu hali iliyopandisha hasira za nyota na kuamua kubadili matumizi ya uwanja.

Katika mchezo huo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Azam Complex Mtibwa ilishinda mabao 2-1 huku timu zote zilicheza mpira wa kasi na kushambuliana kwa zamu huku presha ya mchezo ikiwa juu hali iliyomfanya mwamuzi kuwaonya wachezaji kadhaa kwa kadi ya njano.


Kiungo James Kotei raia wa Ghana alicheza kwa dakika 72 kabla ya kumpisha Mzamiru Yassin ambapo alianza sambamba na nahodha Jonas Mkude ambao walionekana kucheza vizuri na kuifanya safu hiyo kuwa ngumu kwa Wakata miwa.

Huu ni mchezo wa pili wa kujipima nguvu kwa timu ya Simba kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi baada ya juzi kuifunga Polisi Morogoro mabao 2-0 yaliyofungwa na Abdi Banda na Ibrahim Ajib. 

Magoli ya Mtibwa yalifungwa na Stamili Mbonde dakika ya pili baada ya kiungo Musa Ndusha kurudisha pasi fupi kwa mlinda mlango Daniel Agyei huku la pili likifungwa na Jaffar Salum.


Dakika ya 82 ShaabanNditi  alimchezea rafu Ibrahim Ajibu ndani ya eneo la hatari ambapo mwamuzi aliiamuru ipigwe penati lakini mpira uliopigwa na beki Janvier Bokungu uligonga mwamba kabla ya  wachezaji wa Mtibwa kuokoa.

Post a Comment

 
Top