BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally
UKITAJA mabeki wenye roho za 'kikatili' uwanjani basi huwezi kumuacha beki wa zamani Azam FC, Said Morad. Ni beki ambaye uwanjani ni matata asiyekubali mshambuliaji ampite kirahisi na kutikisa nyavu zao ingawa yeye anasema ubabe huishia uwanjani kupigania timu akitoka hapo maisha ya nje ya uwanja yanaendelea kama kawaida kama ni kwenda 'kugonga mvinyo' inakuwa poa zaidi.

Morad kwasasa yupo huru anasaka timu baada ya kuachwa na matajiri wa Ligi Kuu ya Vodacom nchini, alifanya jaribio la kwanza la kutua Singida United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL) jaribio ambalo alilipiga chini alipoona halina faida kwake.

Morad ambaye amecheza VPL kwa zaidi ya miaka 11 akipitia timu za Ashanti United, Simba, Kagera Sugar na Azam FC amezungumza mambo mbalimbali na BOIPLUS kuhusiana na soka lake ambayo ni; KUONDOKA AZAM FC
Kukaa bila kazi kuna changamoto kubwa kwa mtu yoyote labda kwa mfanyabiashara ambaye amezoea kujiajiri na si yule aliyezoea kuajiriwa. Hii ni changamoto inayomkumba Morad aliyeachwa na Azam FC msimu uliopita.

"Sijawahi kukumbana na changamoto kubwa kama kipindi hiki ambacho sina timu, mpira ndiyo ajira yangu sasa nisipocheza inakuwa shida. Nilipokuwa Azam niliingiza pesa na sio sasa nipo tu ndiyo maana maisha yamebadilika, waliniacha dakika za mwisho nikiwa sina namna ya kwenda timu nyingine, siwezi kuzungumzia zaidi hilo kwani lilikwishatokea naangalia mbele.

"Ila kwa ufupi maisha ya Azam yalikuwa mazuri pamoja na changamoto ndogondogo zilizokuwepo, maana hata usipocheza kuna zile posho maisha yalikuwa yanakwenda tofauti na sasa hivi," alisema Morad.


SINGIDA UNITED
"Nilisaini mkataba wa mwaka mmoja na Singida United ila sikuwahi hata kwenda kutokana na mambo ambayo yalijitokeza baina yangu na wao. Maana unakwenda sehemu ukitegemea unalipwa kiasi fulani cha fedha, bahati mbaya haikuwa hivyo ndiyo maana niliomba tuvunje mkataba ili niwe huru na wao walikubali sasa maisha yanaendelea.

"Ningejisikia furaha sana kucheza FDL maana ndiko nilikotokea na huku chini ndiko chimbuko langu, najuwa ugumu na urahisi wa ligi, sheria za soka ni zile zile, kikubwa tu ni kwamba ulinzi uimarishwe kwenye mechi za FDL," MAFANIKIO
Morad anaanika mafanikio yake na wapi ameyapata, "Nimepita sehemu mbalimbali ila sikupata mafanikio kama nilivyopata Azam nimeweza kujenga nyumba zangu mbili na kununua maeneo sehemu mbalimbali, hilo ni jambo kubwa kwangu kwamba niliweza kukumbuka kupata mahali pa kulala halafu mengine yafuate.

"Mbali na hayo nimechangia Azam kutwaa vikombe mbalimbali, ubingwa wa VPL na ubingwa wa Kombe la Kagame na furaha zote ambazo Azam walizipata na mimi nikiwepo, ushirikiano wetu ulifanya tupate mafanikio hayo, nilifanikiwa pia kununua gari lakini niliuza na kufanya jambo lingine naamini nitalipata tu kwani jambo la msingi nimemaliza kulifanya ambalo ni nyumba," alisema Morad.


'10 PERCENT'
Wachezaji wengi wamekuwa wakilalamika ingawa malalamiko yao ni ya chini chini kuhusu kuombwa asilimia fulani kutoka kwenye fedha zao za usajili maarufu kama 10 percent na viongozi wa klabu husika ila kwa Morad ni tofauti.

"Pesa yangu ambayo hulipwa kwenye timu huwa inakuwa yangu mwenyewe, sijawahi kukumbana na hali hiyo pengine hao viongozi huwa wanaangalia  mchezaji mwenyewe ni wa aina gani, nimeenda Simba, Kagera kote huku sijawahi hata kujaribiwa,".USHINDANI 
Wanasema kila mtu ana mbabe wake, ndivyo ilivyokuwa kwa Morad alikutana na wababe kibao ingawa hata yeye alikuwa anawafanyia ubabe wenzake. Alipotua Simba alikutana na wachezaji ambao tayari wamejihakikishia namba na kuwatoa lazima ufanye kazi ya ziada ingawa nyakati zake zilikuwa ni zile zama za akina Juma Nyosso na Meshack Abel.

"Simba ndiyo kulikuwa na muziki mnene ilikuwa huwezi kufika na kuingia kikosini kama sasa hivi, niliowakuta wote wakongwe na wapo kwenye kiwango bora hivyo ilinibidi niwe mpole tu na kujifunza vitu kutoka kwao, kiukweli walinijenga sana maana kwa mchezaji mwenye umri mdogo huwezi kufanya ujinga.

"Hata nilipotua Azam nilimkuta Joseph Owino na wengine, ilinichukuwa muda lakini nashukuru kocha Stewart Hall kwa kipindi hicho alinielewa na hivyo kuanza kunitumia pamoja na Aggrey Moris ambaye alinijengea kujiamini zaidi,"


NIDHAMU 
"Mchezaji anatakiwa afuatiliwe kwenye mpira wake na sio maisha, kikubwa kinachotakiwa kuangaliwa ni juu ya kazi uliyompa kama anaifanya kiustadi na ufasaha haya maisha ya nje yasiingiliwe kwani ni maisha binafsi, yaingiliwe endapo kazi aliyopewa hafanyi.

"Kila mtu ana hulka yake ila asihukumiwe kwa hulka zake ingawa pia mchezaji naye anapaswa kujitambua kwa yale yote anayofanya, pia wanapopata pesa wakumbuke kuwekeza sehemu hasa kwenye ardhi na kujenga kwani kuna maisha baada ya mpira, leo hii nisingejenga ningeishi wapi? Maisha yangu yangekuwa magumu zaidi, nashukuru nilikumbuka kufanya hilo,".


UBORA WA VPL
Morad anasema ligi ya msimu huu ni nyepesi kwa kile alichokiona kwamba timu nyingi zimeruhusu magoli mengi; "Ukiona timu hairuhusu magoli mengi hapo ligi inakuwa ngumu lakini kwasasa ni nyepesi sana,".


ADHABU KWA WACHEZAJI
Morad amelezea kuwa hivi sasa mambo yapo wazi kwani mechi zinapochezwa huonyesha moja kwa moja na vituo vya televisheni hivyo mashabiki huona matukio mengi yanayoendelea, hivyo mchezaji akifanya kosa ni rahisi kuonekana.

"Kuna adhabu nyingine inaweza kutolewa ambayo ni wazi inamuumiza mchezaji na kumrudisha nyuma kwani mchezaji ajira yake ni soka, akipewa adhabu kubwa inamuathiri, hivyo viongozi wetu wajaribu kulitazama hilo kwa wachezaji, waonewe huruma maana sisi bado ni masikini," alisema Morad.


KULINDA UMAARUFU
"Kupata umaarufu ni kazi rahisi sana ila ugumu upo kwenye kutunza huo umaarufu, wengi huwa wanafeli hapo. Ili ufanikiwe kutunza basi ni lazima ujiheshimu, kuangalia maisha yako wapi umetoka na uendapo, kujitunza na upo hatua gani. Hii ni kwasababu kipindi hiki kila mchezaji anataka kuwa maarufu, unaweza kujikuta umaarufu wako unapotea ndani ya msimu mmoja anaibuka mwingine,".MECHI NGUMU
"Nakumbuka mechi kama mbili ambazo zilikuwa ngumu sana kwangu kutokana na upinzani uliokuwepo, mechi ya fainali ya Kombe la Kagame ambapo tulitwaa ubingwa kwa kuwafunga Gor Mahia iliyokuwa na nyota kama Olunga na Allan Wanga walionisumbua sana na pia ile mechi ya Taifa Stars dhidi ya Harambee Stars kwenye Kombe la Chalenji, sitazihau hizo mechi," alisema.

Post a Comment

 
Top