BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR

SIMON Msuva wa Yanga huenda akawa amechochea moto wa winga wa Simba, Shiza Kichuya baada ya kumfikia mabao aliyofunga hapo jana wakati timu yake ilipocheza dhidi ya Ruvu Shooting na kuibuka kwa ushindi wa bao 3-0. Mechi hiyo ilichezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kichuya ndiye mchezaji aliyekuwa akiongoza kwa mabao tisa hadi mzunguko wa kwanza unamalizika lakini sasa amefikiwa na Msuva mwenye mabao kama hayo ingawa Kichuya anatarajia kuingia uwanjani jioni ya leo Jumapili kucheza na Ndanda Fc ya Mtwara.

Kichuya huenda akaingia kwa kasi mpya baada ya kuona wapinzani wamemfikia kwa idadi hiyo ya mabao na kufanya kila jitihada ya kufunga kwenye mechi hiyo itakayochezwa Uwanja wa Nangwanda.

Kama Kichuya atafanikiwa kutikisa nyavu leo kwa bao lolote atakalofunga basi ataendelea kumtimulia vumbi Msuva na asipofanikiwa basi ushindani kwake utaendelea kuwa mkubwa.Wakati nyota hao wakichuana kwa mabao hata timu zao zinapigana vikumbo kukaa kilele kwani Simba ndiyo ilikuwa ikiongoza kwa pointi 35 hadi mzunguko wa kwanza unamalizika na ushindi wa jana kwa Yanga umeishusha Simba nafasi ya pili. Yanga wamefikisha pointi 36.

Yanga wanaendelea kuwaombea mabaya watani zao hao ili wapoteze mechi ya leo ama kutoka sare tu.

Post a Comment

 
Top