BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar
Simon Msuva kushoto akipongezwa na Deus Kaseke (katikati) na Haruna Niyonzima

WINGA Simon Msuva amezifanya Yanga na Simba 'zisafiri' uelekeo tofauti kwenye msimamo wa Ligi kuu ya Vodacom baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi Maafande wa JKT Ruvu mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Yanga ambao ni mabingwa watetezi wamefikisha pointi 36 na kusafiri kwenda kileleni mwa msimamo ikiwa ni alama moja mbele ya Simba ambao kesho watashuka kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara kumenyana na Ndanda FC.

Mlinzi wa Ruvu Michael Aidan alijifunga dakika ya 39 katika harakati za kuokoa krosi ya  Msuva aliyepokea pasi ya Haruna Niyonzima kabla ya kuvunja mtego wa kuotea na kuwazidi kasi mabeki wa Ruvu na kumimina krosi hiyo.

Yanga ilirudi kwa kasi kubwa kipindi cha pili kwa kuliandama lango la Ruvu ambapo dakika ya 57 Msuva alifunga bao la pili baada ya kupokea pasi ya Kaseke kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Niyonzima.Msuva tena alifunga bao la tatu dakika za nyongeza baada ya kupokea pasi maridadi ya nyota wa mchezo huo, Niyomzima ambaye aliwapa wakati mgumu sana viungo wa Ruvu.

Mwamuzi Elly Sasii kutoka Dar es Salaam aliwaonya kwa kadi ya njano wachezaji Yusuph Chuma, Edward Charles na Rahim Juma wote wa Ruvu huku Donald Ngoma akipata kwa upande wa Yanga kutokana na mchezo usio wa kiungwana.

Ruvu iliwatoa Atupele Green na Ally Bilal na kuwaingiza Musa Juma pamoja na Saady Kipanga. Yanga iliwapumzisha Amissi Tambwe, Thaban Kamusoko na Ngoma kuwaingiza Saidi Makapu, Geofrey Mwashiuya na Obrey Chirwa.

Post a Comment

 
Top