BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
KLABU ya Mbao imepata udhamini wa Sh 25 milioni kwa mkataba wa miezi sita huku wakipewa sharti moja kwamba wakifanya vizuri wataboreshewa mkataba huo.

Kampuni ya Hawaii Product Suppliers kupitia bidhaa yao ya Cowbell ndiyo wameipa jeuri Mbao FC ya jijini Mwanza ambayo ilikuwa na ukata mkubwa kwenye mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom ambapo wanashika nafasi ya 12 wakiwa wamekusanya pointi 16.

Menaja Masoko wa Kampuni hiyo, Elisalia Ndeta alisema kuwa wameamua kuingia mkataba na Mbao FC kutokana na kuvutiwa baada ya kufanya vizuri mechi za mwishoni kwenye mzunguko huo. 

"Kama watafanya vizuri basi kuna maboresho kwenye mkataba wetu, tumedhamini baada ya kufurahishwa na kiwango chao kwenye mechi za mwisho mwisho mwa mzunguko wa kwanza, tunaamini watafanya vizuri zaidi," alisema Ndeta.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa Mbao FC, Solly Zephania Njashi, aliishukuru kampuni hiyo kwa udhamini wa mechi 15 zilizobaki ambapo fedha hizo zitawasaidia kulipa mishahara wachezaji wao.

"Timu zenye matatizo ya fedha zipo nyingi, tunashukuru kwa udhamini huu ambao tunatakiwa kuutunza, sisi tutajipanga kuhakikisha tunafanya vizuri mechi zijazo ili tuendelee kunufaika na udhamini huu," alisema  Njashi.

Post a Comment

 
Top