BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu, MBEYA
MSHAMBULIAJI Mrisho Ngassa tayari ametua jijini Mbeya jioni hii ya leo na kupokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Mbeya City ambayo amekwenda kukamilisha mazungumzo ya kusaini mkataba baada ya kuachana na Fanja FC ya Oman.

Ngassa ametua jijini humo kwa usafiri wa anga akitumia Ndege ya Shirika la Fastjet huku kocha Kinnah Phiri akisema kuwa ana imani kubwa ya kumalizana vizuri na mchezaji huyo ambaye amemfundisha akiwa timu ya Free State ya Afrika Kusini aliyovunja nayo mkataba.

Imeelezwa kuwa Ngassa atasaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea Mbeya City hivyo kuungana na nyota wapya Zahoro Pazi na kipa Hussein Salum kwa upande wa wachezaji wapya wazawa.

Imeelezwa kuwa Mbeya City pia imemalizana na washambuliaji watatu wa kigeni Tsipa Leonard kutoka Caps United ya Zimbabwe, Waganda Tito Okello, Hood Mayanja pamoja na beki William Otong ambao waliichezea African Lyon mzunguko wa kwanza wa ligi.

"Nafarijika wachezaji wote ni wazuri, napata matumaini mapya ya kwamba mzunguko wa pili tutafanya vizuri, naamini pia Ngassa tutamalizana vizuri kwani ni mchezaji mzuri na ninafahamu uwezo wake," alisema Phiri.

Mbeya City itatangaza kikosi chake muda wowote kuanzia sasa kwani dirisha la usajili litafungwa kesho Alhamisi saa 6:00 usiku.

Post a Comment

 
Top