BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu
MSHAMBULIAJI mpya wa Mbeya City, Mrisho Ngassa leo Alhamisi asubuhi amepata hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC), hivyo huenda kocha Kinnah Phiri akamtumia kwenye mechi yao ya keshokutwa Jumamosi dhidi ya Mbao FC kama hali yake kiafya itakuwa nzuri.

Ngassa jana alishindwa kufanya mazoezi na Mbeya City kwani alikuwa anasumbuliwa na tumbo hivyo kupewa mapumziko ya muda na huenda akawepo kwenye mazoezi ya leo jioni.

Mwenyekiti wa City, Mussa Mapunda  amethibitisha kutua kwa ITC hiyo kutoka Shirikisho la Soka la Oman ikiwa ni siku chache baada ya klabu ya Fanja  kumruhusu Ngassa kujiunga na kikosi cha City.

"Ni kweli tumeipata, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Chama cha Mpira cha Oman, hakika wamefanya kazi kubwa kufanikisha kupatikana kwa ITC  hii na pia naishukuru Fanja Fc na watendaji wote kwenye timu yetu, tumekuwa na mawasiliano mazuri muda wote mpaka tumefanikiwa," alisema Mapunda.

Mapunda alisema kuchelewa kufika kwa ITC hiyo hakukuwa na msuguano wowote baina ya klabu hizo mbili bali kilichotokea ni tofauti ya wakati na siku za ufanyaji kazi  kwenye ofisi kulingana  na taratibu za nchi hizi mbili.

"Hakukuwa na msuguano wowote uliosababisha  kuchelewa kwa ITC ya Ngassa, ni utofauti wa taratibu za kiofisi  mara nyingi Oman siku za Ijumaa na Jumamosi inakuwa ni mapumziko na huku kwetu Jumapili inakuwa mapumziko, hapo ndipo palikuwa panatuletea  mpishano, jambo jema ni kuwa tayari tumeipata na tunaweza kumtumia mchezaji kwenye michezo yote ya ligi na mingine ambayo inaihusu klabu yetu," alisema.

Post a Comment

 
Top