BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

KIUNGO fundi wa timu ya Yanga Haruna Niyonzima 'Fabregas' amewadhihirishia wasomaji wa mtandao wa BOIPLUS kuwa hawakufanya makosa kumchagua mwezi uliopita kuwa kiungo bora aliyeisaidia zaidi timu yake mzunguko wa kwanza.

Katika mechi tano za mwisho za mzunguko huo Niyonzima alikuwa kwenye kiwango bora na kuisaidia Yanga kufanya vizuri kwa kupunguza idadi ya pointi kutoka nane hadi mbili dhidi ya Simba wenye pointi 35 na leo ameisaidia kupaa kileleni mwa msimamo baada ya kufikisha pointi 36.Niyonzima alipata kura 1405 sawa na asilimia 63 na kumshinda kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto aliyepata kura 756 sawa na asilimia 27 ambapo awali alikuwa akiongoza kabla ya raia huyo wa Rwanda kugeuza matokeo na kumwacha kwa kura nyingi.

Katika mchezo wa leo walioibuka na ushindi wa mabao 3-0,dhidi ya JKT Ruvu Niyonzima alionyesha kiwango cha hali ya juu kwa kupiga pasi mbili zilizozaa mabao huku akiwalaza Maafande hao na viatu baada kuwasumbua vilivyo kwa chenga za maudhi.Niyonzima alimpigia pasi safi Simon Msuva aliyepiga krosi iliyomgonga beki Michael Aidan na kuingia wavuni katika jitihada za kutaka kuokoa na kuiandika Yanga bao la kwanza.

Raia huyo wa Rwanda alifanya hivyo tena dakika za nyongeza kwa kutoa pasi maridhawa kwa Msuva aliyefunga bao la tatu baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Ruvu.

Post a Comment

 
Top