BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi Wetu

KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Kinnah Phiri amesema kuwa wachezaji wake wapya Mrisho Ngassa na Zahoro Pazzi ambao wote wamepata ITC zao kesho Jumamosi wanaweza wasiwe sehemu ya kikosi chake kitakachocheza dhidi ya Mbao ama wataanzia benchi.

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya huku akiweka sababu za kutokuwa na uhakika wa kuwatumia nyota hao ni kwamba Ngassa alikuwa anaumwa na amefanya mazoezi mepesi ya siku moja tangu apate nafuu huku Zahoro pia akishindwa kufanya mazoezi kwani alikuwa anafuatilia ITC yake.

"Ngasa na Zahoro hawako fiti asilimia 100, watakuwepo kikosini lakini tunaweza  kuwatumia kipindi cha pili, siku mbili nyuma Ngassa  alikuwa anasumbuliwa na tumbo, leo amefanya mazoezi  mapesi, kwa mujibu wa daktari ni wazi hatuwezi kumtumia muda wote  wa mchezo, hivyo hivyo kwa Pazzi ambaye amefanya mazoezi kwa siku tatu sasa,' alisema Phiri. 


Akizungumzia mechi ya kesho Jumamosi, Phiri alisema kuwa ni muhimu kupata ushindi na amefanya marekebisho ya makosa aliyoyaona katika mechi mbili zilizopita ambazo zote alitoka sare dhidi ya Kagera na Toto Africans zilizochezwa Uwanja huo wa Sokoine.

"Tumejitahidi kurekebisha mapungufu yote yaliyokuwepo kikosini kwenye michezo miwili iliyopita, vijana wangu wako ‘fit’ na wameniahidi kufanya vizuri, ni jambo jema kusikia hivyo kutoka kwao  hii ni kwa sababu kila mmoja anataka  tushinde, wapo wachezaji kadhaa tutawakosa kwa sababu ni wagonjwa, Danny Joram na Omary Ramadhani hawatakuwepo kabisa kikosini," alisema Phiri.

Post a Comment

 
Top