BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, MBEYA
KOCHA mkuu wa Mbeya City, Kinnah Phiri imeanza mzunguko wa pili wa ligi kuu kwa sare tasa huku akiweka wazi kwamba kikosi chake kina mabadiliko  tofauti na mzunguko uliopita ingawa wachezaji wake bado hawajaelewana vizuri kwani wengine ni wageni.

Mbeya City ilishindwa kumpa usumbufu mkubwa kipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja ambaye aliidakia timu hiyo msimu uliopita kwani washambuliaji wa City walipiga mashuti matatu pekee makali ambayo Kaseja aliyapangua huku mengine hayakuwa na malengo yoyote.

Phiri ambaye amefikisha pointi 20 sasa ameiambia BOIPLUS kuwa anakubaliana na maamuzi ya mwamuzi wa pembeni aliyekataa bao lao lililofungwa na Omary Ramadhan dakika ya tatu ambalo lilidaiwa kuwa aliotea. Ramadhan alifunga bao hilo akiunganisha krosi ya Titto Okelo aliyesajiliwa akitokea African Lyon.


Phiri alisema kuwa mechi hiyo ilikuwa nzuri kwao kwani wachezaji wake walicheza vizuri ingawa kuna kasoro ndogo alizoahidi kuzifanyia kazi kabla ya mechi yao ijayo ambayo pia itachezwa kwenye Uwanja wa Sokoine.

"Lengo letu ni kuanza kwa ushindi mechi hii lakini hatujaweza kutimiza hilo, ingawa nikiangalia kikosi changu kwasasa kinanipa faraja kubwa naamini pia wachezaji wengine ni wapya hivyo bado hawajaelewana vizuri, tutajiandaa kwa mechi nyingine," alisema Phiri.

City haikuwatumia nyota wake wapya akiwemo Mrisho Ngassa ambaye walitarajia angeonekana kwenye mechi huku ikielezwa kwamba taratibu za uhamisho hazijakamilisha wakati Zahoro Pazzi akiendelea kufuatilia ITC kutoka FC Lupopo.

Post a Comment

 
Top