BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, DAR

PRISONS jana Jumatatu iliambulia kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Wanajeshi wa Ruvu Shooting matokeo ambayo yameonekana kuwavuruga huku wakitamka kwamba kila kitu kitamaliziwa pale Chamazi watakapocheza na Azam FC keshokutwa Alhamisi.

Kinachowapa kiburi Prisons pamoja na kupoteza mechi hiyo ni kutokana na mwenendo mbovu wa Azam tofauti na misimu iliyopita na mechi iliyopita walitoka sare na Majimaji ikiwa ni sare yao ya pili mfululizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wachezaji wa Prisons walisema kuwa Azam ya sasa ni ya kawaida tofauti na hapo awali ambapo wakikutana ilikuwa mechi ngumu.

"Tunahitaji ushindi, tunahitaji pointi tatu ambazo tutazipata kwao Azam. Azam wamesajili nyota kibao wa kigeni ambao hawana makali yoyote hivyo tumejipanga kuonyesha kuwa sisi tunaweza bila wageni.

"Tunajuwa nao wanajiandaa kwani hawajafanya vizuri lakini maandalizi yao si kwa ligi hii, sasa hivi wamepotea," alisema Salum Kimenya.

Akizungumzia mechi yao na Ruvu Shooting alisema kuwa; "Mabao ya mapema yalituvuruga sana na sijui tumefungwaje, ni matokeo yanayosikitisha maana mechi nzima tumecheza vizuri ila jinsi mabao yalivyofungwa ndio mtihani,".

Kwa upande wa mshambuliaji wao Victor Hangaya alisema kuwa; "Kila mtu anayekwenda kufanya jambo fulani anatarajia matokeo mazuri, ndivyo ilivyokuwa kweli ila wenzetu walifanikiwa kutuotea mapema.

"Tunaelekea kucheza na Azam mechi ambayo sidhani kama nitacheza kwani nimeumia sehemu ya goti na ninasikia maumivu makali sana ila naamini wale watakaocheza watajuwa ni jinsi gani ya kuwabana Azam," alisema Hangaya.

Prisons haijawahi kushinda kwenye Uwanja wa Chamazi zaidi ya kutoka sare mara mbili na mechi nyingine wamekuwa wakipoteza.

Post a Comment

 
Top