BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar

FAMILIA ya mwanasoka Mbwana Samatta anayekipiga katika timu ya KRC Genk ya Ubelgiji imeandaa sherehe maalumu ya kumpongeza mshambuliaji huyo itakayofanyika Januari 7 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.

Awali sherehe hiyo ilipangwa kufanyika mara tu alipopata tuzo ya Mchezaji Bora Afrika, Januari 7 mwaka huu lakini haikufanyika kutokana mshambuliaji huyo kuwahi kwenda kukamilisha mambo yake ya usajili na Genk akitokea TP Mazembe.

Sherehe hizo zitakwenda sambamba na uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na baba yake mzazi, Mzee Ally Samatta kinaelezea maisha ya Samatta tangu akiwa mtoto na alipoanza kujifunza soka kuanzia mkoani Mbeya hadi alipofikia sasa.

Akizungumza na BOIPLUS, Mzee Samatta alisema kuwa katika sherehe hiyo kutakuwepo na mechi ya kirafiki ambayo itazikutanisha timu mbili za ligi kuu Bara ambazo bado wanafanya nazo mazungumzo.


"Kwasasa Samatta yupo jijini ana siku kama tatu ila uhakika wa yeye kuwepo kwenye sherehe hiyo ya kumpongeza ni mdogo kwani ataondoka kwenda Ubelgiji kwenye maandalizi ya mechi zao za michuano ya Europa na ligi kuu nchini humo, kama kutakuwa na mabadiliko basi atakuwepo. Hii tunatimiza ahadi ambayo tulitaka kuifanya tangu alipotwaa tuzo hiyo.

"Kama Samatta atakuwepo basi atakuwa mgeni rasmi vinginevyo tutamualika mwakilishi kutoka serikalini, TFF ama mwakilishi wa taasisi za kijamii maana sherehe hizo zitakwenda sambamba na uzinduzi wa kitabu chake ambacho nimeandika mimi pamoja na Peter Chingole," alisema Mzee Samatta.

Mzee Samatta alisema kuwa kwasasa wanaanza kumpongeza Samatta katika jiji hili la Dar es Salaam lakini wana mpango kwa mwaka mwingine kwenda kufanya shughuli kama hiyo Jijini Mbeya ambako ndiko hasa chimbuko lake lilianzia.

Post a Comment

 
Top