BOIPLUS SPORTS BLOG

BARCELONA, Hispania
KWA mara nyingine beki Sergio Ramos ameibuka shujaa wa Real Madrid baada ya kuinusuru na kichapo dhidi ya mahasimu wao Barcelona baada ya kusawazisha bao dakika za majeruhi na kutoka sare ya bao 1-1 kwenye uwanja wa Camp Nou.

Ramos amekuwa akifunga mabao muhimu dakika za majeruhi ambapo dakika ya 90 alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliochongwa na Luca Modric na kuwafanya Los Blancos kuambulia sare.

Licha Barcelona kumiliki mpira zaidi, Madrid walikuwa bora zaidi kipindi cha kwanza baada ya kufanya mashambulizi kadha langoni mwa Barca lakini safu yao ya ulinzi iliyokuwa chini ya Gerrad Pique na Javier Marsherano ilikuwa imara kuzuia mikikimikiki ya akina Cristiano Ronaldo.


Luis Suarez aliwapatia wenyeji bao la uongozi dakika ya 53 kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Neymar huku beki Rafael Varane akiruka bila mafanikio.

Kiungo fundi Andres Iniesta aliingia dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Ivan Rakitic na kubadilisha ladha ya mchezo ambapo Barca walitulia  na kucheza vizuri huku wakimiliki mpira kwa kiasi kikubwa eneo la kati.

Dakika ya 81 Lionel Messi alipoteza nafasi ya wazi baada ya kupokea pasi kutoka kwa Iniesta na kumpiga chenga Varane lakini shuti lake lilitoka pembeni kidogo ya lango.

Madrid wameendelea kubaki kileleni baada ya kufikisha pointi 34 huku Barcelona wakibaki nafasi ya pili wakiwa na alama 28.

Post a Comment

 
Top