BOIPLUS SPORTS BLOG

Mwandishi wetu

KOCHA wa Maafande wa JKT Ruvu Bakari Shime ameamua kuwapa dozi wachezaji wake kutwa mara tatu ili kujiwinda na mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa ligi dhidi ya mabingwa watetezi Yanga utakaopigwa Disemba 17 kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Shime amechukua nafasi ya kocha Malale Hamsini aliyejiunga na majirani zao Ruvu Shooting baada ya kuwaacha nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi kutokana na kujikusanyia pointi 13 pekee katika mechi 15 za mzunguko wa kwanza.

Ofisa Habari wa Maafande hao Afisa Mteule daraja la pili Constantine Masanja alisema kikosi chao kimeweka kambi kwenye uwanja wa JKT Mbweni ambapo wachezaji, benchi la ufundi pamoja na Uongozi wamedhamiria kuhakikisha wanaondoka mkiani mwa msimamo wakianzia na mchezo wao wa kwanza dhidi ya Yanga.

Masanja alisema Kocha Shime anafurahishwa na wachezaji wake kuitikia na kuelewa mafunzo yake kwa haraka zaidi kitu kinachompa moyo wa kufanya vema katika mzunguko wa pili wa ligi.

"Timu inaendelea vizuri na mazoezi kwenye uwanja wa JKT Mbweni mara tatu kwa siku ili kuwaweka sawa wachezaji kabla ya kuanza duru ya pili ya ligi kwakua tumedharia kufanya vizuri tukianza na Yanga" alisema Masanja.

Masanja alisema Uongozi umempa rungu kocha Shime kuchuja wachezaji wataotumika katika mzunguko wa pili huku akiridhishwa na nyota wa kikosi cha vijana ambao anatarajia kuwa na mchango mkubwa kwa siku za baadae pamoja na wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha dogo.

Post a Comment

 
Top