BOIPLUS SPORTS BLOG

Sheila Ally, Dar
DIRISHA la usajili linafungwa leo saa 6:00 usiku huku Simba ikigonga mwamba hadi muda huu kumnasa beki wa kulia wa Mtibwa Sugar, Ally Shomary baada ya uongozi wa klabu hiyo ya Manungu kugoma kumwachia.

Simba ilifanya mazungumzo ya awali na mchezaji huyo baada ya kushindwa kumalizana na beki wa Prisons, Salum Kimenya aliyetaka asajiliwe kwa Sh 40 milioni ili aachane na ajira yake wakati uwezo wa Simba ni Sh 30 milioni.

Baada ya kushindwa kufanikisha usajili huo sasa Simba itabaki na wachezaji wake Janvier Bokungu na Hamad Juma huku mabeki wa kati imeelezwa kuwa Abdul Banda atachukuwa nafasi ya Juuko Murshid ambaye yupo na timu yake ya Taifa ya Uganda inayojiandaa na fainali za Afcon. 

Habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa, uongozi wa Simba unapambana kuona ni jinsi gani Juuko ataongezwa mkataba mpya kwani mkataba wa sasa unamalizika mwezi ujao lakini wakigonga mwamba kuwashawishi Mtibwa juu ya Shomary ambaye mara kadhaa wanazungumza naye.

"Tulizungumza na uongozi wa Mtibwa Sugar lakini imeonyesha bado wanamuhitaji Shomary hivyo mpango ulishindikana tutabaki na hawa hawa waliopo sema kocha anaweza kubadilisha kikosi hasa mabeki wa kati," alisema kiongozi huyo.

Kwa upande wa Shomary alikiri kufanya mazungumzo hayo ila maamuzi aliwaachia viongozi wake, "Walinifuata tukazungumza lakini niliwaambia wakamalizane kwanza na viongozi wangu, wakikubali ningeondoka lakini hadi sasa sijaambiwa lolote, Simba wanachelewa wenyewe kwani mara nyingi wananifata ila wanaishia kuzungumza tu,".

Post a Comment

 
Top