BOIPLUS SPORTS BLOG

Bakari Kagoma, Dar

SIMBA kwani wanajali....wamejipigia JKT Ruvu bao 1-0 hivyo kuwa wamekusanya jumla ya pointi 41 na kuwaacha watani zao Yanga kwa pointi nne jambo ambalo huenda limewaudhi sana kwani wao wanapointi 37.

Mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ambapo matokeo hayo ni kama zawadi ya Sikukuu ya Krismasi kwa mshabiki wa Simba huku Yanga wakiwa wanaendelea kuiwaza sare yao ya bao moja dhidi ya African Lyon iliyowatibulia mahesabu yao ya kukaa kileleni.

Mashabiki wa Yanga huenda walikuwa wakiiombea Simba kupoteza ama kutoka sare mechi ya leo ili wasiachwe kwa pointi nyingi lakini Simba inayoonekana kuwa na uchu wa kutwaa ubingwa walipambana kuhakikisha Maafande hao hawaleti madhara langoni mwao.

Mshambuliaji mpya wa Simba Pastory Athanas alicheza vizuri kipindi cha kwanza na kuwafanya mabeki wa Ruvu waliokuwa chini ya Frank Nchimbi na Yusuph Chuma kuwa makini naye kutokana na utulivu anapokuwa langoni na umahiri wa kulazimisha kuingia ndani ya eneo la hatari na kupiga krosi.


Pastory Athanas akiwatoka walinzi wa JKT Ruvu

Mzamiru Yassin aliifungia Simba bao la pekee kipindi cha kwanza kwa kichwa baada ya kumalizia mpira wa krosi uliopigwa na Pastory huku kipa wa Ruvu akiwa chini baada ya kuumia wakati mpira ukiendelea bila kuchukua tahadhari.

Kipindi cha pili Ruvu walifunguka zaidi na kutaka kusawazisha bao hilo kwa kufanya mashambulizi langoni mwa Simba lakini safu ya ulinzi ya Wekundu hao ilikuwa imara zaidi huku mshambuliaji Athanas akiendelea kuwasumbua mabeki wa Maafande hao kwa mashambulizi ya kushtukiza.

Mwamuzi Hans Mabena kutoka Tanga aliwaonya kwa kuwaonyesha kadi ya njano Edward Joseph na Aziz Gilla wa Ruvu huku James Kotei na Jonas Mkude wakipewa kwa upande wa Simba.

Kocha wa Simba, Joseph Omog alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Bokungu, Mohamed Ibrahim na Kotei na kuwaingiza Hamad Juma, Jamal Mnyate pamoja na Said Ndemla wakati Ruvu iliwapumzisha Ally Bilaly, Gilla na Mussa Juma nafasi zao zilichukuliwa na Najim Magulu, Atupele Green na Kassim Kisengo.

Matokeo ya mechi zingine zilizochezwa leo;
Kagera Sugar 1-0 Stand United
Ndanda 0-2 Mtibwa
Majimaji 1-1 Azam
Mwadui 1-0 Mbao
Mbeya City 0-0 Toto Africans

Post a Comment

Yorram Mabugas said... 24 December 2016 at 19:38

Siyo kwel bana pass ya goli haikupigwa na bukungu Bali na athanas, bukungu aliudokoa mdog ndipo athanas akaumimina golin na mzamiru kutia majalo huku bek w jkt aking'aang'aa sharubu bila kujua nn cha kufany

 
Top